Uholanzi na Uganda wamekubaliana kushirikiana kuhusu waomba hifadhi ya kisiasa waliokataliwa kupitia Uganda kwa muda, serikali ya Uholanzi ilisema katika taarifa siku ya Alhamisi.
Waziri wa Uhamiaji na Mambo ya Nje wa Uholanzi David van Weel na mwenzake wa Uganda Odongo Jeje Abubakhar wametia saini barua ya makubaliano jijini New York, wanapohudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mpango huu utatumika tu kwa raia ambao nchi zao ni karibu na Uganda na wanaotakiwa kuondoka Uholanzi lakini hawawezi kurejea katika mataifa yao moja kwa moja kwa kipindi fulani. Wataruhusiwa kukaa Uganda kwa muda kabla ya kurudi katika nchi zao.
'kudhibiti uhamiaji'
"Tunachukuwa hatua hii pamoja na Uganda ili kudhibiti uhamiaji. Bila shaka haki za msingi za wale wanaorudi kwao kupitia Uganda zitalindwa," Van Weel amesema, akiongeza kuwa serikali ya Uholanzi inapanga kushauriana kwa karibu na Umoja wa Ulaya na taasisi za kimataifa, kama vile IOM na UNHCR.
Mwezi Machi, tume ya Ulaya ilipendekeza kuruhusu nchi wanachama kuweka vituo vya wahamiaji katika nchi ambazo si wanachama wa EU kwa wale waliokataliwa hifadhi ya kisiasa.
Uhalali wa sheria hii kwa Uholanzi na sheria ya kimataifa haufahamiki.
Maelfu ya waomba hifadhi ya kisiasa
Uhamiaji itakuwa suala muhimu katika uchaguzi wa Uholanzi wa mwezi ujao, kufuatia kusambaratika kwa serikali ya sasa ya muda mwezi Juni kutokana na kutofautiana katika sera za uhamiaji.
2024, waomba hifadhi 32,175 waliingia Uholanzi, ikiwa ni idadi ya chini kwa asilimia 16 ikilinganishwa na 2023.