Mgogoro wa Mashariki ya Kati hasara kwa mauzo ya nyama Kenya
AFRIKA
3 dk kusoma
Mgogoro wa Mashariki ya Kati hasara kwa mauzo ya nyama KenyaWawekezaji katika sekta  ya nyama wanasema usafirishaji wa nyama kutoka Kenya hadi nchi za uarabuni, umeshuka hadi chini ya asilimia tano ya viwango vinavyotarajiwa kusafirishwa kwa kawaida.
Sekta ya nyama nchini Kenya inapata hasara kutokana na mzozo wa Mashariki ya kati / REUTERS
tokea masaa 2

Mzozo wa Mashariki ya Kati umepunguza kwa kiasi kikubwa mauzo ya nyama kutoka nchini Kenya kwenda Mashariki ya Kati hasa katika msimu huu wa Ramadhan ambapo mauzo kwa kawaida huwa ya juu.

Mashambulizi yaliyoanzishwa Februari 28, 2026 na Marekani akishirikiana na Israel dhidi ya Iran, yalisababisha Iran nayo kulipiza kwa kushambulia nchi za Ghuba zinazohodhi kambi za Marekani, hivyo kuathiri biashara baada ya nchi za Ghuba kufunga anga zake.

Katika machinjio ya Kaunti ya Kiambu, uzalishaji umepungua baada ya majokofu kujaa nyama.

Hali inayowafanya wafanyabiashara kuhangaika kuhamisha nyama ili kutoa nafasi kwa nyama nyengine kuhifadhiwa.

Nicholas Ngahu ni Mtendaji Mkuu wa Baraza la Wasafirishaji wa Nyama na Mifugo nchini Kenya.

"Tumeathirika sana kama wauzaji wa nyama, tunauza chini ya asilimia kumi na tano ya mauzo yetu ya kawaida, na sasa ni Ramadhan, tunauza chini ya asilimia tano ya malengo yetu," anaelezea Ngahu.

Wawekezaji katika sekta  hiyo wanasema usafirishaji wa nyama kutoka Kenya hadi nchi za Uarabuni, umeshuka hadi chini ya asilimia tano ya viwango vinavyotarajiwa kusafirishwa kwa kawaida.

Mashariki ya Kati ndio soko kuu la nyama kutoka Kenya, huku Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE ikinunua hadi asilimia 60.

Saudi Arabia, Oman, Qatar, na Kuwait pia ni wateja wakubwa.

Kabla ya mashambulizi kuanza, mwishoni mwa Februari, Kenya ilikuwa katika hali ya kuongeza mauzo na mapato yake ya nyama Mashariki ya Kati.

Jumla ya mauzo ya nyama ya Kenya yalipanda kutoka zaidi ya $88.9M (Sh11.5 bilioni mwaka wa 2022) hadi zaidi  ya 146.9M (Sh19 bilioni) mwaka wa 2023 na $139.1M (Sh18.7 bilioni) mwaka 2024, hii ikionesha wastani wa ukuaji wa kila mwaka.

Kushuka kwa kasi kwa mauzo ya nje kumechangiwa na ongezeko la gharama za usafirishaji wa ndege na ada ya bima baada ya mashirika mengi ya ndege yanayohudumia eneo hilo kupunguza safari zake za kawaida na hapo kuwalazimu wauzaji wengine kutegemea ndege binafsi za mizigo kwenda Falme za Kiarabu, ambayo gharama yake ni kubwa.

“Tuna wasiwasi kuwa baada ya Ramadhan vita vikiendelea hatutakuwa na biashara kabisa kwa maana uwezo wa wateja kuhitaji nyama sana utakuwa imepungua sana. Katika kipindi cha Ramadhan ndio wananunua nyama zaidi, lakini baada ya Ramadhan siku za kawaida biashara zetu zinapungua kwa kawaida,” Denis Muraya, Afisa wa usafirishaji mizigo anasema.

Wasafirishaji wa nyama ya ng'ombe, kondoo na mbuzi kwa sasa wanaweza kutuma kiasi kidogo sana Abu Dhabi na Dubai, wakati usafirishaji kwenda Oman, Kuwait, Bahrain na Jordan unaendelea kutatizwa.

Wizara ya Kilimo ya Kenya inasema kuwa nchi hiyo ilikuwa ikituma nyama na bidhaa za wanyama nchi za Ghuba zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 2.3 kila wiki.

Wasiwasi mkubwa hivi sasa ni kutojua lini mzozo huu utafikia tamati.

CHANZO:TRT Swahili