Hatua ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Nassir, ya kutangaza azma ya kupiga marufuku matumizi, usafirishaji na uuzaji wa muguka imezua mjadala mpana nchini Kenya, ikifungua mjadala mzito kuhusu mipaka ya mamlaka ya serikali za kaunti, sera za afya ya umma na uhalali wa kisheria wa zao hilo.
Gavana Nassir amesema muguka ni “tishio kubwa kwa afya ya vijana” na haina manufaa yoyote ya kitabibu, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda afya ya umma ndani ya Kaunti ya Mombasa.
Kauli hiyo inakuja licha ya uamuzi wa Rais wa Kenya, William Ruto, aliyefuta marufuku ya awali ya uuzaji wa muguka mwezi Mei 2024 na kutangaza kuwa biashara ya mmea huo ni halali kisheria chini ya sheria za kitaifa.
Muguka ni nini?
Muguka ni aina ya miraa (khat), mmea unaotafunwa ukiwa mbichi kwa madhumuni ya kusisimua akili. Hupandwa zaidi katika maeneo ya mashariki mwa Kenya, hususan Embu, na husafirishwa kwa wingi hadi maeneo ya Pwani.
Bei yake nafuu na upatikanaji wake rahisi—kuanzia shilingi 50 za Kenya—umechangia kuenea kwake kwa kasi, hasa miongoni mwa vijana wa mijini.
Ingawa matumizi ya miraa yana historia ya kitamaduni katika baadhi ya jamii za Afrika Mashariki, wataalamu wa afya wanaonya kuwa matumizi ya muguka kwa kiwango kikubwa na cha muda mrefu yameleta athari mpya na changamano za kiafya na kijamii, hususan katika mazingira ya mijini.
Athari kwa Mtindo wa Maisha na Vijana
Katika Mombasa na maeneo mengine ya Pwani, matumizi ya muguka yameathiri kwa kiasi kikubwa ratiba za kila siku, mahusiano ya kifamilia na ushiriki wa vijana katika elimu na ajira.
Walimu na wanaharakati wa kijamii wanasema matumizi hayo yamechangia kuongezeka kwa utoro shuleni, kushuka kwa ufaulu na kuenea kwa tabia hatarishi miongoni mwa wanafunzi.Bakari Mohammed, mwalimu katika Shule ya Alidina, anasema madhara ya muguka yanaonekana wazi shuleni.
“Wanafunzi hulala darasani kwa sababu muguka husababisha kukosa usingizi. Matokeo ya masomo hushuka na tabia hubadilika; kijana aliyekuwa mpole anaweza kuwa mkali na asiyeheshimu wakubwa zake kwa sababu akili imeathirika,” anasema.
Kwa mujibu wa NACADA, eneo la Pwani limeathirika zaidi na matumizi ya muguka ikilinganishwa na dawa nyingine za kulevya, huku vijana wakiwa kundi linaloathirika zaidi.
Simulizi za Waathirika
Miongoni mwa waathirika ni Alawy Hussein (sio jina lake halisi), aliyekuwa mraibu wa muguka na sigara. Anasema alikumbwa na matatizo makubwa ya afya ya akili hadi kupatikana akihangaika mitaani.
“Muguka imetuharibu sana sisi vijana wa Mombasa. Niliokolewa barabarani nikiwa sijielewi, nikitembea uchi. Imenivuruga akili. Naomba serikali ipige marufuku muguka kabisa.”
Mwingine ni Sofia Omari (sio jina lake halisi), ambaye kwa sasa anapatiwa matibabu ya afya ya akili. Anasema uraibu ulimfanya ashindwe kutekeleza majukumu ya ulezi na kuharibu maisha ya familia.
“Nilishindwa kabisa kulea mtoto wangu. Nilikuwa naondoka kuomba pesa ili nikanunue muguka. Imeniharibia maisha yangu, naomba iondolewe kabisa.”
Mzigo kwa Mfumo wa Afya ya Akili
Vituo vya kurekebisha tabia na hospitali za afya ya akili katika Kaunti ya Mombasa vimeripoti ongezeko la wagonjwa wanaohusishwa moja kwa moja na matumizi mabaya ya muguka.
Amina Mohammed, msimamizi wa Mombasa Women Empowerment Centre, anasema wagonjwa wengi walioko chini ya uangalizi wao wameathiriwa na matumizi ya muda mrefu ya muguka.
“Tunapowachukua barabarani, mara nyingi tunawakuta na mafurushi ya muguka. Familia zao husema walianza kutafuna taratibu, kisha wakaanza kuchanganya na vitu vingine hadi afya ya akili ikaharibika.”
Taib Basheib, Mkurugenzi wa Reach Out Centre Trust, anasema tatizo la muguka ni kubwa zaidi kuliko linavyoonekana.“Kwa tathmini zetu, karibu asilimia 100 ya watumiaji wa muguka tunaokutana nao wako katika hali mbaya—wanaishi mitaani au wana matatizo makubwa ya akili, hasa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 25.”
Madhara ya Kiafya
Madaktari wanaeleza kuwa muguka ina kemikali za cathinone na cathine, ambazo husababisha msisimko wa muda mfupi na hisia za furaha.
Jalab Ashraf, mtaalamu wa afya, anasema matumizi ya muda mrefu yana madhara makubwa:“Huathiri mdomo na meno, husababisha vidonda vya tumbo, kuvimbiwa, kukosa usingizi, wasiwasi na sonona. Kwa muda mrefu, inaweza kusababisha kupoteza akili au wazimu.
”Wataalamu wanaonya kuwa athari hizi huongeza mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya ya umma, hasa katika maeneo yenye rasilimali chache.
Changamoto za Kisheria na Msimamo wa Bunge la Kaunti
Wachambuzi wa sera wanasema marufuku ya ngazi ya kaunti inaweza kukumbana na changamoto za kisheria, ikizingatiwa kuwa serikali kuu imetangaza muguka kuwa halali.
Hata hivyo, Katiba ya Kenya inaruhusu serikali za kaunti kuchukua hatua za kulinda afya ya umma ndani ya mipaka yao.
Frankline Makanga, diwani wa Wodi ya Chaani na mjumbe wa Kamati ya Afya katika Bunge la Kaunti ya Mombasa, anasema suala la muguka linapaswa kushughulikiwa kama dharura ya afya ya umma, si hoja ya kisiasa.
“Hili si suala la kufanya siasa. Kadri muda unavyosonga, vijana wetu wanazidi kuumia. Muguka inasababisha kukosa usingizi na inaathiri afya ya akili kwa njia nyingi,” anasema.
Anasema Bunge la Kaunti litaiomba idara husika kuandaa sera mahsusi kuhusu mazao na bidhaa zinazofaa kuuzwa ndani ya Mombasa, huku akitoa wito kwa Bunge la Taifa kuiondoa muguka kwenye orodha ya mazao ya biashara.
Mitazamo Tofauti ya Kiuchumi
Si wote wanaounga mkono marufuku hiyo. Githinji Tatu, mfanyabiashara wa muguka, anasema kudhibiti ni bora kuliko kupiga marufuku kabisa.
“Muguka iendelee kuuzwa lakini iwekwe sheria kali za kudhibiti. Marufuku si suluhisho, kwa sababu wengi wetu tunategemea biashara hii kwa riziki,” anasema.
Hitimisho
Kadri mjadala kuhusu mustakabali wa muguka unavyoendelea, athari zake kwa vijana, familia na mfumo wa afya zinazidi kujitokeza wazi.
Wataalamu wanakubaliana kuwa tiba ya uraibu ipo, lakini wanasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya umma, kinga na sera shirikishi zitakazoweka afya ya jamii mbele ya maslahi ya kisiasa na kiuchumi.Swali linalosalia ni iwapo hatua za serikali ya kaunti zitafanikiwa kulinda afya ya vijana—au kama mgongano wa kisera kati ya kaunti na serikali kuu utaendelea kudhoofisha juhudi za kukabiliana na tatizo hili.


.jpg?width=720&format=webp&quality=80)


.jpg?width=128&format=webp&quality=80)












