Kundi la muqawama la Palestina Hamas litawaachilia mateka wote wa Israel huko Gaza mnamo Oktoba 13, Rais wa Marekani Donald Trump alisema.
Trump alizungumza na familia za mateka wa Israel kwa njia ya simu siku ya Jumatano, kufuatia tangazo la kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza.
Jamaa wa mateka hao walitoa shukrani zao kwa Trump kwa juhudi zake katika kufikia makubaliano hayo.
Wakati wa simu hiyo, Trump alisema kuwa mateka wote wa Israel wataachiliwa siku ya Jumatatu.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, rais wa Marekani alisisitiza kwamba mateka 'WOTE' wa Israeli wataachiliwa.
Hata hivyo, Trump hakubainisha iwapo kuachiliwa huko kutajumuisha miili ya mateka waliofariki dunia.
Awali Trump alitangaza kuwa Israel na Hamas wametia saini katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya Gaza yaliyopendekezwa na Marekani.
Mpango huo wenye vipengele 20, uliotangazwa kwa mara ya kwanza tarehe 29 Septemba, unajumuisha kuachiliwa kwa mateka wote wa Israel kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina, kusitishwa kwa mapigano, kupokonywa silaha kwa Hamas, na kuijenga upya Gaza.
Tangu Oktoba 2023, mashambulizi ya Israel yameua takriban Wapalestina 67,200 katika eneo hilo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Mashambulio hayo ya mara kwa mara yameifanya Gaza kuwa bila watu, na kusababisha njaa na magonjwa.