Familia ya marehemu balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa, Nathi Mthethwa, imeelezea ujumbe wa mshikamano kutoka kote Afrika Kusini na nje ya mipaka kuwa ni “faraja katika majonzi” kufuatia kifo cha balozi huyo mjini Paris wiki hii.
Mthethwa alifariki baada ya kuripotiwa kuanguka kutoka ghorofa ya 22 ya hoteli moja mjini Paris. Alikuwa akihudumu kama balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa tangu Disemba 2023, baada ya kuwa na taaluma ndefu ya kisiasa iliyojumuisha nyadhifa kadhaa za uwaziri kati ya mwaka 2008 na 2023.
Katika taarifa ya pamoja, familia za Mthethwa na Buthelezi zilisema kuwa kifo cha Mthethwa kimeacha “pengo ambalo haliwezi kuelezeka kwa maneno.”
“Katika kipindi hiki cha majonzi makubwa, familia za Mthethwa na Buthelezi zinatoa shukrani za dhati kwa wingi wa upendo na mshikamano kutoka kote Afrika Kusini na nje ya mipaka… Hata hivyo, ujumbe wenu wa rambirambi umeleta faraja katika huzuni yetu, ukitukumbusha kuwa hatuko peke yetu,” ilisomeka taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa familia, Dkt. Sfiso Buthelezi.
‘Faraja katika huruma’
Familia hizo pia zilitoa shukrani kwa serikali ya Afrika Kusini kwa msaada wao wakati wa kipindi hiki cha maombolezo, shirika la habari la serikali SABC liliripoti.
“Tunapongoja ufafanuzi zaidi, tunapata faraja katika mshikamano na huruma iliyodhihirishwa na Waafrika Kusini kutoka kila tabaka la maisha — wakiomboleza nasi, wakiheshimu kumbukumbu ya Nathi, na kutambua huduma yake ya maisha yote kwa taifa letu,” taarifa hiyo iliongeza.
Familia ilisema itashirikiana kwa karibu na Idara ya Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano (DIRCO) ili kurudisha mwili wa Mthethwa nyumbani.
Familia ilisema mara taratibu rasmi zitakapokamilika, itashirikiana kwa karibu na serikali kuleta mwili wa Nathi nyumbani kwa ajili ya mazishi “yanayostahili urithi wake.”
Baada ya kuripotiwa kupotea Jumatatu, Nkosinathi Emmanuel Mthethwa alipatikana amefariki nje ya Hoteli ya Hyatt mjini Paris, waendesha mashtaka walisema.
Kifo cha balozi huyo kimezua mshtuko mkubwa na maombolezo kimataifa na katika nchi yake ya nyumbani.