Mamlaka za Syria ziliamua kuongeza muda wa kupiga kura katika Damascus na miji mingine mikubwa nchini humo Jumapili, wakati wa uchaguzi wa bunge wa kwanza tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al Assad.
“Upigaji kura umeongezwa muda katika Damascus na miji mikubwa katika baadhi ya majimbo, huku vituo vya vijijini Damascus na maeneo mengine vikiwa vimefungwa,” alisema Mohammed al Ahmad, mkuu wa Kamati Kuu ya Uchaguzi wa Bunge la Syria, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari vya serikali.
Alisema mchakato huo “unaendelea kwa utulivu, na Wasyria wanajivunia kushuhudia uzoefu wao wa kwanza wa kweli wa kuchagua wawakilishi wa Bunge la Watu.”
Rais Ahmed al Sharaa alifika katika kituo cha kupigia kura cha Maktaba ya Taifa huko Damascus kushuhudia mchakato wa uchaguzi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Macho yote kwa matokeo
Kulingana na Shirika la Habari la Syria (SANA) na kituo cha utangazaji cha umma Al-Ikhbariya, wagombea 1,578 wanashindania viti 210 katika Bunge la Watu, ambapo wanawake wanawakilisha asilimia 14 ya wagombea.
Takriban theluthi moja ya viti vinateuliwa moja kwa moja na rais, huku theluthi mbili zilizobaki zikichaguliwa na “mashirika ya uchaguzi” yaliyoteuliwa katika kila wilaya.
Waangalizi kutoka kwa balozi za kidiplomasia na mabalozi waliothibitishwa walikuwepo katika kituo cha Maktaba ya Taifa kufuatilia uchaguzi huo.
Msemaji wa Kamati ya Uchaguzi, Nawar Najma, alisema upigaji kura ulipangwa awali kumalizika saa 6 mchana kwa saa za ndani (0900GMT) lakini unaweza kuongezwa hadi saa 10 jioni (1300GMT) ili kuwapa nafasi wapiga kura wote waliohitimu.
Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa katika mkutano wa waandishi wa habari Jumatatu au Jumanne.
Tangu kuondolewa kwa Assad mwishoni mwa 2024, serikali mpya ya mpito ya Syria imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kisiasa na kiuchumi huku ikihimiza mshikamano wa kijamii na kupanua ushirikiano na washirika wa kikanda na kimataifa.
Assad, aliyekuwa kiongozi wa Syria kwa karibu miaka 25, alikimbilia Urusi Desemba iliyopita, na kumaliza utawala wa Chama cha Baath ambacho kilikuwa madarakani tangu 1963. Utawala mpya wa mpito wa Al Sharaa uliundwa Januari.