Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema kuwa hatua ya Israel kuzuia msafara wa Global Sumud Flotilla ni "kosa kubwa" dhidi ya "umoja wa kimataifa na hisia zinazolenga kupunguza mateso huko Gaza."
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Ramaphosa alitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa raia wa Afrika Kusini na wanaharakati wengine wa kimataifa waliodaiwa kukamatwa katika maji ya kimataifa walipokuwa wakijaribu kufikisha msaada kwa Wapalestina.
“Kwa niaba ya serikali yetu na taifa, naiomba Israel kuwaachilia mara moja Waafrika Kusini waliotekwa katika maji ya kimataifa, na kuwaachilia raia wengine waliokuwa wakijaribu kufika Gaza na msaada wa kibinadamu,” alisema Ramaphosa.
Msafara huo, uliokuwa na meli kadhaa zilizobeba misaada ya kibinadamu, ulikamatwa na vikosi vya Israel walipokuwa wakikaribia Gaza.
“Hatua hii pia inakiuka amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inayosema kuwa msaada wa kibinadamu lazima uruhusiwe kupita bila kuzuiwa,” alisema Ramaphosa, akiongeza kuwa msafara huo uliashiria "umoja na Gaza, siyo uhasama na Israel."
Ramaphosa alisisitiza kuwa operesheni kama hiyo inakiuka sheria za kimataifa, uhuru wa mataifa mbalimbali, na amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki inayotaka msaada wa kibinadamu upelekwe Gaza bila vizuizi.