Maafisa wa polisi wa Kenya waliokuwa nchini Haiti chini ya misheni ya kulinda amani wanarejea nyumbani.
Hii inafuatia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha Kikosi kipya cha kimataifa cha Kupambana na Magenge (GSF) nchini Haiti kuchukua nafasi ya ujumbe wa usaidizi wa usalama unaoongozwa na Kenya.
Magenge yenye silaha yamechukua udhibiti wa karibu katika mji mkuu wote wa Haiti Port-au-Prince katika mzozo ambao umewalazimu takriban watu milioni 1.3 kuacha makazi yao, na kuchochea njaa kwa kiwango kikubwa.
Kenya ilikuwa ikiongoza ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama (MSS), ulioidhinishwa na Baraza la Usalama mnamo Oktoba 2023.
Imekuwa Haiti kwa mwaka sasa
Kikosi hicho kilikuwa na takriban maafisa 1000 wa polisi huku Kenya ikichangia zaidi ya polisi 600.
Wengine walitoka Bahamas, Belize, El Salvador, Guatemala na Jamaica. Makubaliano ya kutumwa Haiti yalikubaliwa na rais William Ruto chini ya utawala wa aliyekuwa rais wa Marekani Joe Biden.
Lakini utawala wa Donald Trump sasa umependekeza mbinu mpya ya kuwa na kikosi cha maafisa 5,500 na Umoja wa Mataifa umeidhinisha.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, chini ya mamlaka ya awali ya miezi 12, kikosi kipya kitafanya kazi kwa uratibu wa karibu na Polisi wa Kitaifa wa Haiti na vikosi vya jeshi la Haiti kufanya operesheni zinazoongozwa za kijasusi ili kupunguza magenge, kuleta utulivu na usalama wa miundombinu muhimu, na kusaidia ufikiaji wa kibinadamu.
Kikosi hicho chenye wanajeshi 5,550 pia kitalinda makundi yaliyo hatarini, kusaidia kuunganishwa tena kwa wapiganaji wa zamani na kusaidia kuimarisha taasisi za Haiti.
Kikosi kipya bado kitategemea michango ya hiari ya wafanyakazi na ufadhili, lakini muundo wa uongozi utakuwa tofauti.
Kitaongozwa na kundi la wawakilishi kutoka nchi ambazo zimechangia wafanyakazi, pamoja na Marekani na Canada.
Kikosi hicho pia kitaungwa mkono na ofisi mpya ya Umoja wa Mataifa.
Rais wa Kenya William Ruto aliuambia Umoja wa Mataifa wiki jana kwamba ujumbe huo umetatizika na ufadhili.
Alisema magari ni machakavu, hivyo yameharibika sana.Mpaka sasa, tayari Kenya imepoteza maafisa watatu katika kikosi chache huko Haiti.
Haijabainika ikiwa ujumbe unaoongozwa na Kenya utaingizwa katika kikosi kipya ambacho kimependekeza. Kenya imeelezea nia yake ya kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya amani nchini Haiti .