Serikali ya Kenya imethibitisha kwa mara ya kwanza kuuliwa kwa Mkenya Okoth Ogutu kwa kupigwa risasi wakati wa machafuko ya hivi karibuni ya baada ya uchaguzi nchini Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, alisema serikali inachukua hatua zote muhimu kuchunguza mazingira yaliyosababisha kifo cha John Okoth Ogutu, mwenye umri wa miaka 33 aliyekuwa mwalimu akiishi na kufanya kazi nchini Tanzania.
“Ni tukio la kusikitisha lililotokana na hali ya vurugu iliyokuwepo. Tumewasiliana na maafisa walioko Dar es Salaam. Ninapenda kuihakikishia familia kwamba kesi hii itashughulikiwa kwa njia ya heshima,” alisema Katibu huyo.
Kauli hiyo imekuja huku familia ya marehemu ikionyesha kuchoshwa na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi, wakidai wamekuwa wakizungushwa bila majibu wanapojaribu kupata msaada wa kurejesha mwili wa ndugu yao nyumbani.














