Waandamanaji nchini Madagascar siku ya Jumamosi waliingia Uwanja wa Mei 13 mjini Antananarivo kwa mara ya kwanza tangu maandamano yalipoanza mwezi uliopita, wakiwa chini ya ulinzi wa kijeshi.
Maandamano hayo yalianza Septemba 25 kutokana na uhaba wa maji na umeme, lakini yameongezeka na sasa yanatoa changamoto kubwa kwa utawala wa Rais Andry Rajoelina tangu kuchaguliwa tena kwake mwaka 2023.
Mapema Jumamosi, baadhi ya wanajeshi kutoka kikosi cha jeshi kilichosaidia Rajoelina kuchukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 2009 waliwataka wanajeshi wenzao kupuuza amri na kuunga mkono maandamano yanayoongozwa na vijana, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Kikosi maalum cha CAPSAT, ambacho kilikuwa na jukumu muhimu katika kupanda kwa Rajoelina madarakani, kilitoa wito wa nadra kwa umma kuonyesha mshikamano na waandamanaji wanaotaka ajiuzulu.
Wanajeshi waondoka kambini
Video zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wanajeshi wa CAPSAT wakiwataka wenzao "kuunga mkono wananchi."
Viongozi wa kijeshi, wakiwemo mkuu wa majeshi na afisa mwandamizi kutoka Wizara ya Vikosi vya Ulinzi, waliwataka wanajeshi kushiriki katika mazungumzo na majadiliano.
Video iliyotangazwa na vyombo vya habari vya ndani ilionyesha baadhi ya wanajeshi wakitoka kambini na kuwasindikiza waandamanaji kuingia Uwanja wa Mei 13, eneo ambalo limekuwa kitovu cha machafuko mengi ya kisiasa, na ambalo lilikuwa limezingirwa na ulinzi mkali wakati wa ghasia.
Wamtaka rais ajiuzulu
Waandamanaji wanamtaka Rajoelina ajiuzulu, aombe msamaha kwa nchi, na avunje seneti pamoja na tume ya uchaguzi.
Wiki iliyopita, alifuta baraza lake la mawaziri na kumteua waziri mkuu mpya.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 22 wameuawa na 100 kujeruhiwa katika machafuko hayo. Hata hivyo, serikali ya Madagascar imepinga takwimu hizo, huku Rajoelina akisema wiki hii kwamba watu 12 walifariki katika maandamano hayo.