Mfalme Mohammed VI wa Morocco amesema kuboresha elimu ya umma na huduma za afya ni kipaumbele, lakini hakutaja harakati za vijana ambazo zimekuwa zikifanya maandamano kote nchini kwa ajili ya kudai mageuzi makubwa ya kijamii.
Vijana hao wametangaza kusitisha maandamano kwa muda siku ya Jumamosi lakini wamesema madai yao bado hayajabadilika.
"Tumeweka kama vipaumbele... uundaji wa ajira kwa vijana, na kuboresha kwa vitendo sekta za elimu na afya," alisema mfalme katika hotuba yake ya kila mwaka wakati wa ufunguzi wa kikao cha bunge siku ya Ijumaa.
Hotuba ya kifalme ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na waandamanaji, ambao wamekuwa wakikusanyika mitaani karibu kila usiku tangu Septemba 27.
Machafuko hayo yamechochewa na ripoti za hivi karibuni za vifo vya wanawake wanane wajawazito katika hospitali ya umma mjini Agadir, jambo ambalo wakosoaji wanaliona kama dalili ya mfumo unaoshindwa kufanya kazi.
Kombe la Dunia 2030
Wamorocco wengi pia wameonyesha kuchoshwa na matumizi ya fedha za umma wakati Morocco inaendelea na miradi mikubwa ya miundombinu kwa maandalizi ya Kombe la Dunia la 2030, ambalo itashirikiana kuandaa pamoja na Ureno na Uhispania.
Mfalme alisisitiza kuwa "hapapaswi kuwa na mgongano au ushindani kati ya miradi mikubwa ya kitaifa na programu za kijamii."
Serikali ilitoa wito mpya siku ya Alhamisi kwa ajili ya mazungumzo na waandamanaji, ikisema "ujumbe wao umefika" na kuahidi "kufanya kazi haraka kuhamasisha rasilimali na kushughulikia mapungufu."
Mikusanyiko hiyo imekuwa ya amani kwa kiasi kikubwa, ingawa baadhi ya usiku kumekuwa na matukio ya vurugu na uharibifu wa mali.