Nyumba zenye kufuga kasuku, mara nyingi zinahusishwa na utajiri na maisha ya kifahari. Na Afrika imebahatika kuwa mwenyeji wa aina ya kasuku ambaye ni maarufu zaidi.
Katika zaidi ya aina 10 ya ndege hawa barani Afrika, kasuku wa Kiafrika wenye rangi ya kijivu anajulikana zaidi hasa kwa kuwa ni kati ya ndege wenye akili zaidi duniani. Kwa sasa anajulikana kama kasuku wa kijivu au kasuku wa kijivu wa Congo.
Ana rangi ya kijivu na nyeusi, na manyoya mekundu mkiani. Ana uzito wa gramu 400 na anaweza kuwa na urefu hadi kufikia sentimita 33.
Jinsia zote mbili zina muonekano sawa. Utafiti wa kasuku wa Kiafrika wa kijivu umeonyesha kuwa aliyekomaa ana kiwango cha akili sawa na mtoto mchanga.
Utafiti pia umegundua kuwa kasuku hawa wanaweza kutambua, kuomba, kukataa, kuainisha, na kuhesabu zaidi ya vitu 80 tofauti, na kujibu maswali kuhusu dhana ya rangi na umbo.
Kasuku wa kijivu wanapatikana hasa Afrika Magharibi na Kati ikiwa ni pamoja na Angola, Cameroon, Congo, Gabon, Ivory Coast na Ghana.
Katika Afrika Mashariki wanapatikana Kenya, Uganda na Kaskazini-magharibi mwa Tanzania.
Katika makazi yao ya asili, kasuku wa Kiafrika wa kijivu wanaweza kusafiri hadi kilomita 10 kwa siku.
Ndege hawa kawaida wanakuwa na jike mmoja tu, ikiwa na maana kwamba, wao huwa katika mahusiano na jike mmoja kwa wakati mmoja.
Wanataga mayai mara moja hadi mbili kwa mwaka, kuanzia mayai matatu hadi matano yenye umbo la duara, moja kila baada ya muda wa siku mbili hadi tano.
Majike wanapotaga huwa wanalishwa na madume huku wakitunza mayai yao kwa takriban siku thelathini na vifaranga hutoka kwenye kiota wakiwa na umri wa wiki kumi na mbili.
Wana uwezo wa kutoa takriban sauti 200 tofauti, na wanawasiliana karibu kila mara wanapotafuta chakula.
Wanaishi wastani wa miaka 60, na ndege wengine hufikia umri wa miaka 80, kwa hiyo mara nyingi huishi zaidi ya binadamu wanaowamiliki.Hata hivyo, ndege hawa sasa hivi wapo na changamoto ya kutoweka.
Wataalamu wa wanyamapori wanasema hadi asilimia 21 ya kasuku wa mwituni huwindwa kila mwaka ili kusambaza biashara haramu ya wanyamapori, kutokana na mahitaji yao.
Kasuku wa Kiafrika wa kijivu ana soko kubwa hasa Ulaya, Marekani na Mashariki ya Kati ambako wanaonekana kama ndege wa kuvutia kutokana na maisha yao marefu, uwezo wa kuiga sauti za binadamu na uwezo wao wa kufikiri kama binadamu.
Katika masoko kimataifa, kasuku anaweza kuuzwa kati ya dola 250 hadi 5,000 na kumtunza itakugharimu kati ya dola 115 na $265 kwa mwezi.
Wakiwa katika mazingira ya nyumbani, chakula chao kikubwa ni alizeti na pilipili.
Licha ya kuwa ni ndege maarufu anayefugwa, Kasuku wa Kiafrika wa kijivu hata hivyo anapenda zaidi kuwa katika makazi yake ya asili.