Wanajeshi wanne wa Nigeria wameuawa na wengine watano kujeruhiwa wakati vikosi hivyo vikikabiliana na magaidi huko Ngamdu, katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno, jeshi lilisema siku ya Ijumaa.
Makundi ya kigaidi Boko Haram na kundi lenye uhusiano na Daesh mwaka huu yamekuwa yakilenga kambi za wanajeshi katika jimbo la Borno.
Katika shambulio la hivi karibuni siku ya Alhamisi, magaidi walitumia makombora, ndege zisizokuwa na rubani zenye silaha wakilenga wanajeshi na magari yao, msemaji wa jeshi alisema.
Walilenga njia wanayotumia wanajeshi
Magaidi walitega mabomu katika njia wanayotumia wanajeshi ya Ngamdu–Damaturu, na kusitisha shughuli za wanajeshi kwa muda.
Baadaye wahandisi wa jeshi waliondoa mabomu yaliyokuwa yametegwa, na kufungua njia kwa ajili ya wanajeshi kupita.
Jeshi linasema limewauwa washambuliaji wasiopungua 15.
Magaidi wamekuwa wakifanya mashambulizi kadhaa kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka huu, kulingana na data zilokusanywa na shirika linalofuatilia migogoro la ACLED.
Jeshi la Nigeria linasema limeanzisha operesheni maalum ya kukabiliana na magaidi katika miezi ya hivi karibuni kwenye jimbo la Borno kwa lengo la kusambaratisha mitandao ya magaidi kanda ya kaskazini mashariki.