AFRIKA
2 dk kusoma
Tanzania: INEC yafuta kata 10, yatengua uteuzi wa wagombea saba
INEC imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya tangazo la Serikali Namba 596 na Namba 600 la Oktoba 3, 2025.
Tanzania: INEC yafuta kata 10, yatengua uteuzi wa wagombea saba
Mwenyekiti wa INEC Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele./Picha:WengineEC
tokea masaa 10

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (INEC), imefanya marekebisho ya maeneo ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Marekebisho hayo, ni pamoja na kufuta kata kumi, kutengua uteuzi wa wagombea saba wa udiwani, pamoja na kuhamisha vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 12, 2025, na kutiwa saini na Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, INEC imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya tangazo la Serikali Namba 596 na Namba 600 la Oktoba 3, 2025, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alitangaza marekebisho ya mipaka ya maeneo ya utawala na kufuta kata kadhaa.

Kwa mujibu wa INEC, kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Mishamo, Ikolongo, Ndurumo, na Mtapenda zilizoko katika mikoa ya Katavi na Tabora.

Aidha, INEC imetengua uteuzi wa wagombea saba wa udiwani waliokuwa wameteuliwa katika kata hizo kabla ya kufutwa kwake.

Wagombea hao wote walikuwa wakiiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kulingana na INEC, kufutwa kwa kata hizo kumelazimu kuondoa vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa ndani yake, huku vituo vipya 292 vikiundwa katika kata jirani ili kurahisisha upigaji kura kwa wapiga kura 106,288 waliokuwa wamejiandikisha katika maeneo yaliyofutwa.

“Tume imeanzisha vituo vipya katika maeneo jirani ya kata zilizofutwa ili kuwawezesha wapiga kura kutoka maeneo hayo kushiriki ipasavyo katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Tume imewataka wananchi kufuatilia mabadiliko hayo kwa umakini na kuhakikisha wanajua vituo vyao vipya vya kupigia kura, ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura siku ya uchaguzi.

“Kura yako haki yako, jitokeze kupiga kura,” imesisitiza NEC katika taarifa hiyo.

CHANZO:TRT Afrika Swahili