Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala ya Dodoma, imesema inahitaji muda zaidi wa kutoa uamuzi wa mwisho na usio wa mashaka katika shauri la Kikatiba lililofunguliwa na Mgombea Urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kupinga kitendo cha kuondolewa kwake kuendelea na kampeni za kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwisho wa mwezi huu.
Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa hii leo Oktoba 10 ya iwapo Luhaga Mpina ataendelea na mchakato wa kampeni au la.
Shauri hilo la Kikatiba la ACT WAZALENDO linalosikikizwa na majaji watatu dhidi ya Tume ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali sasa litaamuliwa Oktoba 15 mwaka huu kwa njia ya mtandao, ambapo zitakuwa zimesalia wiki mbili kabla ya tarehe iliyopangwa kufanyika Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, hoja zote za shauri hilo la kikatiba zilishasikilizwa kwa hiyo kipengele kilichobaki ni hukumu ya mwisho.
Upande wa waleta maombi ukiongozwa na Wakili John Seka unasema pande zote zilikuwa tayari kupokea uamuzi wa Mahakama Kuu.