Raia wa Cameroon walianza kupiga kura siku ya Jumapili katika uchaguzi wa rais ambapo mtawala aliyeko madarakani Paul Biya, mtawala mzee zaidi duniani mwenye umri wa miaka 92, anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuendelea kung'ang'ania madaraka kwa miaka 43 licha ya upinzani uliojaa nguvu unaoshinikiza mabadiliko.
Wapinzani wa Biya ni pamoja na msemaji wa zamani wa serikali Issa Tchiroma, 76, ambaye amevuta umati mkubwa wa watu akitaka kusitishwa kwa uongozi wa muda mrefu wa kiongozi huyo mkongwe.
Jitihada ya Tchiroma imepata ridhaa kutoka kwa jukwaa la baadhi ya vyama vya upinzani na makundi ya kiraia.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema kuwa Biya, aliye madarakani tangu 1982, huenda akachaguliwa tena kutokana na udhibiti wake thabiti wa mitambo ya serikali na hali ya mgawanyiko wa upinzani.
Katika mji mkuu, Yaounde, wapiga kura walimiminika huku kukiwa na ulinzi mkali katika kituo cha kupigia kura katika kitongoji cha Bastos karibu na ikulu ya rais, ambapo Biya alitarajiwa kupiga kura yake.
"Natumai itakwenda vizuri, haswa kwa bingwa wangu," alisema mpiga kura mmoja, Patrick Mbarga Mboa, 45, akikataa kusema anamuunga mkono nani.
“Natumai amani na utulivu vitaendelea nchini baada ya uchaguzi,” aliongeza Mboa.
Wakosoaji wa Biya bado wana matumaini kwamba anaweza kuondolewa madarakani baada ya miongo kadhaa ya kudorora kwa uchumi na mivutano katika taifa hilo la Afrika ya Kati lenye watu milioni 30, ambalo ni mzalishaji wa mafuta na kakao.