ULIMWENGU
3 dk kusoma
Mkataba wa kusitisha mapigano Gaza kutiwa saini saa 6, wadhamini ni Uturuki, Misri na Marekani
Hamas itawaachia huru mateka 20 wa Israel na karibu wafungwa 2,000 wa Kipalestina kuachiwa huru kama sehemu ya awamu ya kwanza ya makubaliano hayo.
Mkataba wa kusitisha mapigano Gaza kutiwa saini saa 6, wadhamini ni Uturuki, Misri na Marekani
Moshi unafuka kutoka Gaza, baada ya Rais Trump kutangaza kuwa Israel na Hamas walikubaliana juu ya awamu ya kwanza ya usitishaji vita Gaza. / Reuters
tokea masaa 20

Kutiwa saini kwa makubaliano hayo katika hatua ya kwanza ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Gaza kunatarajiwa kufanyika saa 0900 GMT sawa na saa sita asubuhi kwa majira ya saa za Afrika Mashariki, chanzo kilichoarifiwa kuhusu maelezo ya makubaliano hayo kililiambia shirika la habari la Reuters siku ya Alhamisi.

Usitishwaji wa mapigano unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika eneo la Gaza mara tu mkataba huo utakapotiwa saini, chanzo hicho kiliongeza.

Qatar, Misri, Marekani, na Uturuki zimetia saini kama wadhamini wa mkataba wa amani wa Gaza, The Jerusalem Post iliripoti.

Israel na kundi la muqawama wa Palestina Hamas wamesema wameafiki makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu, awamu ya kwanza ya mpango wa Trump wa kumaliza vita vya Tel Aviv huko Gaza ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 67,000 na kugeuza eneo la Mashariki ya Kati.

Hata hivyo baada ya tangazo kwamba Israel na Hamas wamekubaliana mpango wa kusitisha mapigano, wakala wa Ulinzi wa Raia wa Gaza uliripoti mashambulizi kadhaa katika eneo hilo.

"Tangu kutangazwa jana usiku kwa makubaliano kuhusu mapendekezo ya mfumo wa kusitisha mapigano huko Gaza, milipuko kadhaa imeripotiwa, haswa katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza," alisema mmoja wa maafisa wa shirika hilo, Mohammed Al-Mughayyir, akitaja "msururu wa mashambulizi makali ya anga" katika mji wa Gaza.

Jeshi la Israel, wakati huo huo, lilisema Alhamisi kwamba linaendelea kutumwa katika eneo hilo na kujiandaa kwa hatua zozote za operesheni.

Haya yanajiri huku shirika la habari la Reuters, likinukuu chanzo kilichofahamishwa kuhusu maelezo hayo, liliripoti kuwa mikutano ya baraza la mawaziri la usalama la Israel na serikali kuhusu makubaliano ya Gaza imerudishwa nyuma kwa saa mbili na sasa kufanyika saa 1400 GMT sawa na saa kumi na moja za Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yatajumuisha mambo matatu ya msingi: kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel kwenye mpaka uliopangwa, na kuingizwa kwa misaada inayohitajika Gaza baada ya miaka kadhaa ya vikwazo na vita.

Hamas itabadilishana mateka 20 wa Israel na karibu wafungwa 2,000 wa Kipalestina kama sehemu ya awamu ya kwanza ya makubaliano, chanzo kimoja ndani ya kundi hilo la upinzani kiliiambia AFP.

Mabadilishano hayo yatafanyika ndani ya saa 72 baada ya kutekelezwa kwa makubaliano hayo, chanzo kinachofahamu mazungumzo hayo kilisema.

Mateka hao wa Israel wataachiliwa kwa kubadilishana na Wapalestina 250 waliohukumiwa kifungo cha maisha na wengine 1,700 waliotekwa nyara na Israel wakiwemo watoto na wanawake tangu kuanza kwa mauaji ya halaiki, chanzo hicho kiliongeza.

CHANZO:TRT World and Agencies