Mwanamke wa kiislamu akipita mbele ya askari nchini Ujerumani. / Picha: Getty

Na Hannan Hussain

Imepita mwezi mmoja tangu Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) litoe wito kwa viongozi kujitahidi zaidi "kujenga mazungumzo na kukabiliana na chuki dhidi ya Waislamu," huku kukiwa na ongezeko la chuki na ghasia dhidi ya Waislamu katika mataifa ya Ulaya.

Licha ya mwito huu wa kuchukua hatua, Ulaya haionekani kuwa karibu na kuchukua msimamo wa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu.

Mataifa mengi ya Ulaya yanaendelea kuripoti kuongezeka kwa vitisho dhidi ya jamii za Kiislamu katika nchi kama Norway. Wakati huo huo, kuongozeka kwa kanuni tata inatishia maandamano ya amani ya Waislamu na mikutano nchini Ujerumani.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya pia kinaongeza changamoto, huku vyama vyenye mielekeo mahususi dhidi ya Uislamu vikiwania uwakilishi katika uchaguzi wa bunge wa Umoja wa Ulaya mwezi Juni. Haya yote yanasisitiza haja ya kushughulikia chuki iliyokithiri ya Uislamu barani Ulaya na kuhakikisha ulinzi wa kutosha wa uhuru wa Waislamu dhidi ya chuki na ubaguzi.

Ili kukabiliana na vitisho dhidi ya jamii za Kiislamu, baadhi ya nchi zimejaribu kuchukua hatua ingawaje (zisizoleta manufaa). Hivi majuzi Norway iliamua kuwapa silaha maafisa wake wa zamu kukabiliana na vitisho vilivyoongezeka dhidi ya misikiti, wakati Ufaransa ilianzisha "kikosi cha usalama" kudhibiti marufuku yake ya kuvaa hijabu shuleni.

Hatua kama hizo za kiusalama haziwezi kushughulikia peke yake hali inayoongezeka ya kutengwa miongoni mwa Waislamu, wala kuhakikisha mazingira ya kuvumiliana. Mkakati huo pia unaweza kuleta matokeo mabaya, kwani ubaguzi wa rangi unazidi kuenea miongoni mwa polisi Umoja wa Ulaya, kulingana na ripoti mpya kutoka kwa Shirika la Umoja wa Ulaya kuhusu Haki za Msingi.

Kuna hatari ya nchi za Ulaya kuzidisha jamii wawe dhidi ya Waislamu ikiwa mafunzo yao ya polisi hayatoshughulikia chuki dhidi ya Uislamu, ambayo ni nadra.

Athari ya Gaza

Wakati vita vya Israeli dhidi ya Gaza vikichochea hisia dhidi ya Waislamu katika bara zima, Ulaya inahitaji kuchukua msimamo thabiti kukomesha chuki dhidi ya Uislamu.

Waislamu wakionekena kupeperusha bendera ya Palestina kwenye sherehe ya Eid mjini Naples, Italia. / Picha: Getty.

Kwani, kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio dhidi ya Waislamu tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israeli, huku Brussels kukosa kukosoa mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza.

Mpango mdogo wa EU kukomesha uvamizi wa Israel umeleta madhara makubwa kwa Waislamu wa Ulaya. Wanajamii wanahofia kunyimwa uhuru wa kujieleza, kufanya mkutani, na haki yao ya kuandamana katika nchi nyingi.

Kwa mfano, waandamanaji Waislamu nchini Ujerumani wamekuwa wakikabiliwa vikali na polisi kwa miezi kadhaa, huku asilimia 66 ya Waislamu wa Ufaransa wakiripoti kubaguliwa.

Hatua hizi zinapingana kabisa na madai ya Ulaya kwa kuwa wanaheshimu haki za msingi, uhuru na maadili ya watu wenye matabaka tofauti.

"Umoja wa Ulaya unalaani chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu, kama vile tunavyolaani aina zote za ubaguzi, uhasama na vurugu zinazotokana na dini au imani," kulingana na taarifa ya Umoja wa Ulaya katika Siku ya Kimataifa ya Kupambana na chuki dhidi ya Uislamu mwezi uliopita.

Na bado, Waislamu wengi wa Ulaya wanaendelea kukabiliwa na hali inayoongezeka ya kutengwa nyumbani, na Umoja wa Ulaya hauzingatii sana hisia za Waislamu wakati mashambulizi ya Israeli yanapoendelea.

Inashangaza, ndani na nje ya EU, juhudi nyingi za kupambana na chuki dhidi ya Uislamu zimegubikwa na mabishano na mijadala mikali ya umma. Kwa mfano Ujerumani, ambapo serikali inasisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya Waislamu kwa sababu za kidini au nyinginezo "hayakubaliki kabisa."

Hili halijakomesha uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu kuzidi mwaka jana. Tangu wakati huo, vita vinavyoendelea vya Israel dhidi ya Gaza vimeongeza ongezeko la ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani.

Nje ya EU, Uingereza inajitahidi kuzuia ukosoaji unaoongezeka juu ya ufafanuzi wake mpya wa "itikadi kali".

Serikali imefafanua upya msimamo mkali kama "kukuza au kuendeleza itikadi inayotokana na vurugu, chuki au kutovumiliana," ikiipa uhuru mpana wa kutaja watu binafsi au vikundi kuwa vitisho. Wengi wanaiona kama jaribio la kulenga vikundi vya utetezi wa Waislamu kwa jina la kupambana na chuki dhidi ya Uislamu.

London bado haijaondoa hisia hii kwa pande zote za wigo wa kisiasa. Kwa kuzingatia mielekeo hii, Ulaya inakosa umoja katika kupambana na moja ya changamoto muhimu inayowakabili Waislamu wake.

Kupanda kwa mrengo wa kulia

Kinachotatiza mjadala huo ni vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya vinavyopinga Uislamu.

Wanasiasa wengi katika kambi hii wanaona fursa ya kufaidika na kampeni dhidi ya Uislamu na kuelekeza EU zaidi upande wa kulia. Baada ya yote, Brussels inaelekea kwa uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kwa hamu mwezi Juni, na ECR - kundi la vyama vya Ulaya vyenye siasa kali za mrengo wa kulia - inaongoza kampeni yenye nguvu ya kuongeza uzito wake wa mrengo wa kulia bungeni.

Vyama vilivyo na historia ya chuki dhidi ya Uislamu kama vile "Vox ya Uhispania" na "Brothers of Italy" wa Italia, pia vinatumia mwavuli wa ECR kuwania ushawishi mkubwa bungeni, na hivyo kuibua wasiwasi wa uhasama zaidi dhidi ya Waislamu katika siku zijazo.

Kadhalika kuna wafuasi wengi wanaoipinga Ulaya wanatarajiwa kuongoza katika uchaguzi katika nchi tisa Ulaya, na kutoa nafasi ya kutosha kwa wabunge wenye siasa kali za mrengo wa kulia kuunganisha muungano wa wafuasi wengi na kuungwa mkono na wengi.

Kwa jamii ya Kiislamu ya Ulaya, hizi ni dalili za kutisha. Kwanza, kuwepo kwa watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia bungeni kunaweza kuongeza ushawishi mkali dhidi ya vipaumbele vya Umoja wa Ulaya siku zijazo, ikiwa ni pamoja na juhudi za kupambana na chuki dhidi ya Uislamu.

Zaidi ya hayo, vyama vyenye misimamo mikali yenye mielekeo ya chuki dhidi ya Uislamu vingetaka kuridhisha wafuasi wao, baada ya kutumia miaka mingi kuendeleza msuguano kati ya Uislamu na Magharibi.

Kundi la siasa kali za mrengo wa kulia "Alternative for Germany" (AfD) ni mfano halisi: liliendesha ilani ya kupinga Uislamu miaka iliyopita na sasa ni mojawapo ya vyama vikubwa nchini humo.

Kadiri ushawishi wa mrengo wa kulia unavyoongezeka, inaweza kuwa vigumu zaidi kwa EU kulinda uhuru wa Waislamu. Hili ni jambo muhimu la kuzingatia kwa ajili ya kutengeneza mwitikio wa muda mrefu wa umoja huo kwa chuki dhidi ya Uislamu wakati ambapo ubaguzi, uhasama na ghasia dhidi ya Waislamu zikisalia kukithiri katika bara zima.

Suluhisho

Kuna hatua zinazoonekana Ulaya inaweza kuchukua kukabiliana na Uislamu.

Waislamu wainua mabango dhidi ya Islamophobia nchini Italia. / Picha: AFP

Kwa mfano, viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaweza kufikiria kutoa miongozo mahususi kuhusu uangalizi wa polisi na mahitaji ya mafunzo kwa nchi zote wanachama. Wanapaswa pia kuifanya kuwa ni lazima kwa vitengo vyote vya polisi kuashiria chuki dhidi ya Uislamu kama sehemu ya mafunzo yao.

Zaidi ya hayo, vyama vya mrengo wa kati - kushoto na wa mrengo wa kushoto wa EU vinapaswa kutoa manifesto zinazotofautisha waziwazi uhuru wa kujieleza na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Kitendo hiki kingetokeza tofauti kubwa dhidi ya kauli mbaya na ya chuki inayotolewa na vyama maarufu vya siasa kali za mrengo wa kulia kwa jina la Western Values "maadili ya Magharibi." Kwa mtazamo wa uchaguzi, inaweza pia kuruhusu vyama vya mrengo wa kati kutafuta kura za mamilioni ya Waislamu wa Ulaya wakati vyama vyao vinashindana kurejesha umaarufu bungeni.

EU pia inaweza kusaidia kubadilisha mioyo na akili kwa kutekeleza kampeni za elimu kuhusu Waislamu katika shule, vyuo vikuu na vikao vya kitaaluma. Vitendo hivi vinaweza kusaidia kuondoa dhana potofu, kuangazia miunganisho kati ya kikundi hiki na kikundi kizima, na kusisitiza haja ya kuhimiza kuishi pamoja.

Hatua hizi zinaweza kutumika kama njia ya moja ya kusaidia kupambana na chuki dhidi ya Uislamu kwa uzito unaostahili.

TRT Afrika