Na Emmanuel Oduor
Fikra hiyo inajirudia tena lakini safari hii kwa kujaribu kuwahamisha Wapalestina kwenda Afrika.
Zaidi ya karne moja kabla ya Israel kutekeleza moja ya mauaji ya halaiki mabaya zaidi kutokea dhidi ya Gaza, mataifa ya kikoloni ya Ulaya tayari yalikuwa yanachukulia ardhi za kifamilia barani Afrika kama mali yao ya kugawanya watakavyo.
Mnamo mwaka 1903, Uingereza ilipendekeza kuanzisha makazi huru ya Wayahudi katika eneo kubwa linalopatikana sasa magharibi mwa Kenya. Eneo hilo lilikuwa kubwa zaidi kuliko lile lililotengwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1947 kwa ajili ya kuanzisha taifa la Israel.
Mpango huo, uliojulikana kama "Mpango wa Uganda" kwa kuwa eneo lililokusudiwa lilikuwa karibu na reli ya Kenya-Uganda, ulikaribia kubadili historia ya mabara mawili – Afrika na Asia.
Mpango wa mkoloni
Joseph Chamberlain, aliyekuwa Waziri wa Koloni wa Uingereza wakati huo, alipendekeza eneo la milima ya Uasin Gishu kuwa hifadhi salama kwa Wayahudi wa Ulaya waliokuwa wakikimbia chuki dhidi yao.
Akiwa ametoka ziara ya safari ya reli Afrika Mashariki, Chamberlain alimpa pendekezo hilo Theodor Herzl – mwanahabari na mwanasheria kutoka Austria-Hungary, anayejulikana kama mwanzilishi wa harakati za kisiasa za Uzayuni (Zionism).
Chamberlain alisifu hali ya hewa ya Uasin Gishu kuwa "inayofaa kwa wazungu", na akasema eneo hilo linafanana na baadhi ya sehemu za Uingereza.
Lakini Sare Şanlı, mtaalamu wa historia ya makazi ya Wayahudi Afrika, anakanusha madai kwamba mpango huo ulikuwa na misingi ya kibinadamu.
“Mpango wa 1903 ulikuwa wa ‘hifadhi inayolindwa na Uingereza’, siyo ‘Nchi ya Ahadi’. Hili lilikuwa ni jaribio la kisiasa la Uingereza kuelekeza wahamiaji Wayahudi mbali na Ulaya. Muhimu zaidi, si chaguo la kwanza kwa Wayahudi,” asema Şanlı.
Kwa jamii za wenyeji wa Uasin Gishu, mpango huo ulikuwa wa kuwanyang’anya ardhi yao. Herzl mwenyewe hakukubali mpango wa Chamberlain. Lengo lake kubwa lilibaki kuwa Palestina.
Nini kingeweza kutokea?
Mwanahistoria wa Kenya Joseph Boit, mzaliwa wa eneo hilo, anasema kuwa ikiwa mpango huo ungetekelezwa, historia ya Afrika na Mashariki ya Kati ingekuwa tofauti kabisa.
“Je, sisi watu wa Nandi tungekuwa wapi leo? Wayahudi wangekuwa watawala wapya wa kikoloni?” anauliza Boit.
Herzl aliwahi pia kumtaka Sultani Abdul Hamid II wa Utawala wa Ottoman amruhusu kuanzisha makazi ya Wayahudi Palestina, akiahidi kulipa paundi milioni 20. Licha ya utawala wa huo kuwa na madeni lakini Sultani alikataa kabisa.
Herzl kisha akawageukia Waingereza akapendekeza Cyprus au Sinai, lakini walikataa. Ndipo akapendekeza mpango wa Afrika Mashariki.
Mpango huu ulianza kupata mvuto baada ya mauaji ya Wayahudi (pogrom) huko Kishinev, Moldova, Aprili 1903 – lakini hata tukio hilo halikuweza kuunganisha harakati za Uzayuni kukubali pendekezo la Uingereza.
Mpango uliyopendekezwa
Wenyeji wa Uasin Gishu, ardhi ya kilimo – inayojulikana kama "ghala la chakula" la Kenya na eneo alikotoka Rais William Ruto – hawakujulishwa kabisa kuhusu mpango huo, uliokuwa ukijadiliwa kwenye miji ya mbali ya Ulaya.
Mpango wa Uingereza ulikusudia kuanzisha serikali ya ndani ya Wayahudi, chini ya uangalizi wa koloni. Baraza hilo lingesimamia miundombinu, elimu na polisi, lakini bado likiwa chini ya uangalizi wa wakoloni Waingereza.
Wazungu waliokuwa wamekwisha weka makazi Afrika Mashariki walipinga vikali. Magazeti ya kikoloni yaliandika makala kali dhidi ya mpango huo, wakikiita "Jewganda". Wazungu walikutana Nairobi na kutishia vurugu iwapo mpango huo ungefanywa.
Herzl alijadiliana kwa miezi kadhaa kabla ya kuwasilisha pendekezo hilo kwenye kongamano la Uzayuni Agosti 1903. Hakutarajia kuwa pendekezo hilo lingevunja umoja wa harakati hizo.
“Wanachama wa kongamano la Uzayuni walikataa Mpango wa Uganda, wakisisitiza kwamba Palestina ni nchi yao,” asema Dr Serhat Orakçı kutoka Chuo Kikuu cha Haliç, Uturuki.
Wengine waliona Afrika kama hifadhi ya muda, lakini wengi walikataa.
"Wangewezaje kukubali ardhi ya isiyojulikana ya Afrika ilhali ndoto yao ya kale ilikuwa Zion (Yerusalemu)? Kufikia 1905, mpango huo ulikufa," asema Şanlı.
Ndoto zinazoendelea
Mpango wa Uganda ulitangulia Azimio la Balfour la 1917, ambalo Uingereza iliahidi kusaidia kuanzisha makazi ya Wayahudi Palestina. Lakini hata baada ya azimio hilo, juhudi za kutafuta ardhi Afrika kwa ajili ya Wayahudi ziliendelea.
“Angola ilitajwa, lakini Ureno – mkoloni wa eneo hilo – ilikataa. Mpango wa Madagascar ukajadiliwa miaka ya 1930, lakini haukutekelezeka. Mwaka 1944, Ethiopia ilijadiliwa, lakini Mfalme Haile Selassie alikataa – japo Ethiopia ilikuwa na jamii ya Wayahudi wa Beta Israel,” asema Şanlı.
“Kwa hivyo, kila mpango uligonga mwamba – mara nyingine Wayahudi wenyewe walikataa, na mara nyingine wakoloni walikataa. Katika kesi ya Ethiopia, taifa hilo huru lilikataa kabisa”.
Mpango mpya?
Baada ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba dhidi ya Israel, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa wazi kuhusu nia ya kuifuta Gaza kwa madai ya kulipiza kisasi.
Nchi kadhaa za Afrika – ikiwemo Sudan, Somalia, Sudan Kusini na Uganda – zinatajwa kuwa maeneo yanayopendekezwa kuhamishia Wapalestina waliopoteza makazi, japo serikali zao zinakanusha kuhusika na mpango huo.
Viongozi wa siasa kali nchini Israel wamekuwa wakitaka Wapalestina wafukuzwe kabisa ili kuruhusu upanuzi wa makazi ya Wayahudi Gaza.
Historia inajirudia
Wataalamu wanasema kuwa hali hii inaonesha mtazamo wa kikoloni unaoendelea, ambapo Afrika huchukuliwa kama ardhi tupu ya kupeleka watu wasiotakiwa kwingineko.
“Zaidi ya miaka 100 iliyopita, Afrika ilichukuliwa kama mahali pa kuwaweka Wayahudi. Sasa, tunasikia pendekezo la kuwapeleka Wapalestina huko. Mantiki hiyo hiyo bado ipo. Kwa Ulaya, na sasa Israel, Afrika huonekana kama sehemu ya kutupa matatizo yao,” asema Şanlı.
“Mipango hii inazungumzia zaidi kuhusu Ulaya na Israel – siyo Afrika.”
Mwanachuoni kutoka Afrika Kusini, Jo Bluen, ambaye alisaini barua ya wanasayansi 800 Novemba 2023 iliyotangaza matendo ya Israel kuwa ya mauaji ya halaiki, anataka Afrika ichukue hatua kali zaidi dhidi ya Israel.
Anashauri nchi za Afrika zifunge ubalozi wa Israel, zisitishe uhusiano wa kidiplomasia na wa kibiashara.
“Kufunga ubalozi ni hatua ya chini kabisa. Hatuwezi kuruhusu wauaji wa halaiki kuwa miongoni mwetu,” asema Jo. “Kwa nini watu kama hawa wawe na balozi Afrika?”