Maafisa watatu wa polisi wameuawa na wengine saba kutekwa nyara siku ya Jumapili katika shambulio la silaha Jimbo la Benue nchini Nigeria, maafisa wanasema.
Benjamin Hundeyin, afisa uhusiano mwema wa Polisi nchini Nigeria, alisema katika taarifa kuwa watu wasiojulikana na waliokuwa na silaha waliwalenga maafisa wa polisi katika eneo la Agu.
Hundeyin alithibitisha kuwa maafisa watatu walipoteza maisha wakati wa shambulizi hilo huku saba wakitekwa nyara. Aliongeza kuwa maafisa wa usalama wamepelekwa kwenye eneo hili na washukiwa saba tayari wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Hivi karibuni mashambulizi yameongezeka nchini Nigeria katika maeneo mbalimbali kutoka kwa magenge yenye silaha na makundi ya kigaidi ikiwemo Boko Haram na tawi la Afrika Magharibi la ISIS (Daesh), ambalo pia linajulikana kama Islamic State West Africa Province (ISWAP).
Nchi hiyo pia imekuwa na matukio ya utekaji nyara kwa kudai fidia, licha ya kuwepo kwa hukumu ya kifo kwa uhalifu kama huo.
Watu wenye silaha na magenge mara nyingi yanalenga vijiji,shule na wasafiri, hasa katika kanda za kaskazini, wakiitisha malipo ya fidia.