Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimewaahidi watumishi wa umma nchini Tanzania mishahara ya juu, iwapo kitapata ridhaa ya kuiongoza nchi hiyo, baada ya Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Majimoto, Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Salum Mwalim amesema serikali yake haitoruhusu maeneo ya kazi kugeuka kuwa sehemu za mateso kwa watumishi wa umma.
“Hakuna eneo litakalokuwa la adhabu kwa watumishi wa umma. Mtumishi akipelekwa vijijini, atakuwa na bashasha yake, mshahara wake utakuwa mkubwa zaidi kuliko wa yule anayeishi mjini,” alisema Mwalim.
Mgombea huyo, pia amesema kuwa ana nia ya dhati kwenda kutatua suala la ajira nchini kupitia kilimo.
Hali kadhalika, aliweka msisitizo kwenye kutengeneza barabara zote za uzalishaji.
Tanzania inatarajia kufanya Uchaguzi wake Mkuu Oktoba 29, 2025 ambapo wananchi wa taifa hilo wanatumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi mbalimbali, kuanzia rais, wabunge na madiwani.