Machar amekuwa katika kifungo cha nyumbani tangu Machi, kabla ya kufunguliwa kesi ya uhaini, hata hivyo wakili wake alidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Kufungwa kwa Machar hapo awali imezua hofu ya kurudi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2013 hadi 2018 kati ya wapiganaji wa kabila lake la Nuer na wapiganaji wa kabila la Dinka wanaomuunga mkono Rais Salva Kiir, mpinzani wake wa muda mrefu.
Chama cha Machar cha SPLM-IO kimekanusha mashtaka hayo dhidi yake na watu wengine 20, yanayojumuisha mauaji, uhaini, na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kwa madai ya kuhusika kwao katika uvamizi uliofanywa na wanamgambo wa ‘White Army’ wanaotoka kabila la Nuer, kaskazini mashariki mwa nchi mapema mwaka huu.
Katika mahakama hiyo, Machar alionekana akiwa amevaa suti ya rangi nyeusi na tai ya rangi ya samawati, — hii ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana hadharani tangu alipowekwa katika kizuizi cha nyumbani.
Kesi inaenda kinyume na katiba
Wakili wa Machar, Geri Raimondo Legge, alisema kuwa mahakama inaenda “kinyume na katiba, haramu, batili na isiyo na uhalali wowote,” kwa sababu Machar bado ana kinga ya kikatiba kama makamu wa rais aliye madarakani.
Watu saba waliokuwa washirika wa karibu wa Machar, akiwemo waziri wa mafuta, walifunguliwa mashtaka pamoja naye mapema mwezi huu.
“(Tunaomba mahakama) iamuru kuachiliwa mara moja kwa Mheshimiwa Riek Machar Teny, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, pamoja na washitakiwa wengine saba kwa sababu walikamatwa na kuwekwa kizuizini kinyume cha katiba,” Legge aliiambia mahakama.
Mwendesha mashtaka, Ajo Ony’Ohisa Igele, alipinga hoja za upande wa utetezi akizitaja kuwa “hazina msingi na dhaifu.”
Serikali inamtuhumu Machar kwa kuunga mkono kikundi cha White Army — kundi la wanamgambo wa kabila la Nuer,— wakati wa mapigano dhidi ya jeshi la serikali katika mji wa Nasir, kaskazini mashariki, mwezi Machi. Katika machafuko hayo, raia kadhaa waliuawa na zaidi ya watu 80,000 walikimbia makazi yao.
Salva Kiir na Machar, wote wakiwa katika miaka ya 70, walikuwa wakihudumu katika serikali ya mseto yenye mivutano, iliyoundwa baada ya makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Machar, ambaye ni mwanamapinduzi wa zamani, amekuwa na uhusiano wa kutatanisha na Kiir kwa zaidi ya miaka thelathini.