| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Rais Samia wa Tanzania atoa pole kifo cha William Lukuvi
Kulingana na taarifa hiyo, Lukuvi amefariki dunia asubuhi ya Machi 25, 2026 katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Rais Samia wa Tanzania atoa pole kifo cha William Lukuvi
William Lukuvi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Tanzania. / TRT Afrika Swahili
tokea masaa 2

Mbunge wa Jimbo la Isimani na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) nchini Tanzania, William Lukuvi amefariki dunia.

Kifo cha Waziri Lukuvi kimetangzwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa nchi hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo, Lukuvi amefariki dunia asubuhi ya Machi 25, 2026 katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu.

"Tumepoteza kiongozi shupavu, mahiri, mwenye uzoefu mkubwa, mzalendo na mtumishi wa umma aliyelitumikia Taifa letu kwa uadilifu, weledi na kujitolea. Mchango wake mkubwa katika ujenzi na maendeleo ya Taifa letu utaendelea kuenziwa na kukumbukwa siku zote,' ameandika Rais Samia kupitia ukurasa wake wa X.

Wakati huo huo, Rais Samia ametoa pole kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu, familia, wananchi wa Jimbo la Isimani, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Watanzania wote kwa msiba huo.

Kufuatia msiba huo, Spika wa Bunge Mussa Azzan Zungu aliwatangazia wabunge kuahirishwa kwa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge kwa siku hiyo ya tarehe 25 Machi, kwa ajili ya maombolezo.

“Shughuli za Kamati zimeahirishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 176 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Agosti, 2025,” ilisema sehemu ya taarifa ya Bunge kwa Umma.