Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambae pia ni mgombea urais kupitia chama tawala nchini humo CCM amewaasa vijana na wananchi wa taifa hilo kuhakikisha kuwa wanalinda amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
"Vijana twendeni tukalinde amani yetu. Tusikubali kwa hali yoyote, kuswawishiwa kuharibu amani yetu. Hamtakwenda kwenye kuchimba, hamtakwenda kwenye mziki, hamtafanya chochote amani ikiharibika," alisema Rais Samia katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
Rais Samia ambae licha ya kumaliza muhula wake ambao ameuongoza kufuatia kifo cha mtangulizi wake, hii ndio mara yake ya kwanza kupeperusha bendera ya chama hicho kwa lengo la kuomba ridhaa ya kuongoza tena taifa hilo lenye wapiga kura zaidi ya milioni 34.
Mitandao ya kijamii
Kauli ya Rais Samia, inafuatia kampeni zinazoendelea nchini humo kupitia mitandao ya kijamii ambazo zinahamasisha baadhi ya watu kutopiga kura na badala yake, kujitokeza kwa lengo la kufanya maandamano kama njia moja wapo ya kuishinikiza serikali kufanya mabadiliko ya kiutawala pamoja na kuanzisha mchakato wa katiba mpya.
Kwa upande wake, serikali kupitia vyombo vyake vya dola, imewatahadharisha wananchi dhidi ya kujihusisha na vitendo ambavyo vinaweza kuvunja amani, huku ikiahidi kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kufanya hivyo.
Hata hivyo, kadri siku za kuelekea Uchaguzi Mkuu zinavyokaribia, baadhi ya wanaharakati pamoja na wananchi wa nchi hiyo, kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, wanaendelea kuonyesha hasira kali hasa kufuatia tukio la madai ya kutekwa kwa aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole.
Madai ya kutekwa
Taarifa za madai ya kutekwa kwa Polepole na watu wasiojulikana, ziliaza kusambaa juma lililopita. Kufutia taarifa hiyo, Polisi nchini humo kupitia Msemaji wake David Misime, imesema kuwa endelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini ukweli wa kilichotokea.
Polepole ambae miezi kadhaa iliyopita alijiuzulu kutoka wadhifa wake wa ubalozi, na kuanza kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali na viongozi wengine.
Wadau walaani
Tukio hili linaonekana kuibua hisia kali ndani na nje ya Tanzania huku Wabunge wa Umoja w Ulaya (EU) wakililaani na kusema ni tukio la kutisha.
“Tunatoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha usalama wa Polepole na kuchukua hatua madhubuti kumaliza mwenendo wa vitisho na ukiukwaji wa haki za binadamu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kauli hiyo inafuatia matamko kadhaa ambayo yametolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ambayo imeitaka serikali kuchunguza kwa kina hali ya kutoweka kwa Polepole.
Wakati huo huo, wapo wanaoelekeza lawama kwa serikali, kwa madai kwamba, hawaoni hatua madhubuti zikichukuliwa kukabiliana na vitendo vya utekaji ambavyo vinaonekana kushamiri nchini humo.
Lakini mmoja wa wanasiasa maarufu kutoka Chama cha Mapinduzi Christopher Ole Sendeka, ameitetea serikali na kusema tuhuma hizo sio za kweli.
"Lawama zinazoelekezwa ni kana kwamba serikali ina kundi la watu ambao kazi yao ni kuteka. Sasa kama wangekuwa wanateka wale wanaokosoa si hata mimi ningetekwa kama kuna mtu ameikosoa chama hiki, serikali hii, mimi ni mmoja. Kwa hiyo nataka kusema hivi, hatukubaliani na utekaji wa mtu yoyote lakini nadhani ni muhimu kujua nani wanaofanya hivi," amesema Ole Sendeka mbunge wa zamani wa Simanjiro.
Hatma ya Polepole
Mpaka sasa hatma ya Polepole haijafahamika, huku mama yake mzazi ambae aliwahi kuhojiwa na moja ya vyombo vya habari nchini humo, ametaka mtoto wake kuachiliwa huru, na iwapo atakuwa ameuliwa, basi apewe maiti yake akaizike mwenyewe.