Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonya siku ya Ijumaa kuwa kurejea tena “kwa mazingira ya mauaji ya halaiki” Gaza yatakuwa “hatari zaidi,” wakati akieleza kuridhishwa na makubaliano ya kusitishwa mapigano kati ya Israel na Hamas.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa kati ya Israel na Hamas siku ya Alhamisi huko Sharm el-Sheikh nchini Misri, kwa kuzingatia mpango wa mapendekezo 20 yaliyowasilishwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Awamu ya kwanza ya mpango huo inajumuisha kusitishwa mapigano mara moja, kuachiliwa huru kwa mateka na wafungwa, Israel kuondoa majeshi yake kwenye mpaka uliokubaliwa Gaza, na kufikishwa kwa misaada kwa watu wa Gaza, pamoja na msaada wa jamii ya kimataifa katika ujenzi upya wa eneo hilo.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua miradi mipya katika mkoa wa Bahari Nyeusi wa Rize, Erdogan amesema Uturuki imefanya — na itaendelea kufanya — kila iwezalo kurejesha amani, usalama, na uthabiti Gaza “haraka iwezekanavyo.”
‘Hakuna tena umwagikaji damu’
Akieleza kuhusu makubaliano ya kusitishwa mapigano, Erdogan alisisitiza kuwa “kilicho muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa makubaliano hayo yanatekelezwa kikamilifu,” akiongeza kuwa Uturuki itachangia pakubwa katika mchakato huo.
“Kanda yetu, na hasa Gaza, imestahmili umwagikaji damu wa kutosha, mauaji ya kikatili, na majonzi,” amesema. “Amani lazima ipewe nafasi, hatua zozote za kukiuka makubaliano ziepukwe.”
Erdogan alieleza makubaliano hayo kama “hatua kubwa” katika kufikia amani ya kudumu licha ya changamoto zilizopo mbele. “Mlango wa kupatikana kwa amani ya kudumu Gaza umefunguliwa,” alisema. “Tunasema — hakuna tena umwagikaji damu.
Marekani imethibitisha kuwa jeshi la Israel limekamilisha awamu ya kwanza ya kuondoka hadi kwenye mstari wa njano. Chini ya makubaliano hayo, Hamas inatakiwa kuwaachiliwa huru mateka 20 na kurejesha miili 28, huku Israel ikiwaachilia huru wafungwa wa Palestina 250 waliohukumiwa vifungo vya maisha na 1,700 waliokamatwa tangu Oktoba 7, 2023.