Uturuki imemteua Balozi Mehmet Gulluoglu kama Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu kwa Palestina kusimamia shughuli za misaada ya kibinadamu katika eneo la Gaza na kuhakikisha uratibu na taasisi husika na mamlaka za mitaa, vyanzo vya kidiplomasia vimesema Alhamisi.
Gulluoglu atafanya ukaguzi ili kubaini vifaa vya misaada ya kibinadamu na vipaumbele vinavyohitajika huko Gaza, kuratibu na mashirika ya Umoja wa Mataifa na kusaidia shughuli zao huko Gaza, na kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumwa kutoka Uturuki vinawasilishwa kwa wale wanaohitaji huko Gaza kwa njia ya ufanisi zaidi, walisema.
Gulluoglu atatekeleza majukumu yake kwa uratibu na taasisi husika za Kituruki zinazofanya kazi katika sekta hio, kushauriana na mamlaka za mitaa kuhusu msaada utakaotumwa kupitia Misri na Jordan, na kuimarisha usaidizi wa shughulu za afya za Uturuki kwa Gaza, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wagonjwa, vyanzo viliongeza.
Msaada wa kibinadamu wa Uturuki kwa Gaza
Uturuki ina utamaduni thabiti wa usaidizi wa kibinadamu. Uturuki, ikiwa katika eneo linalokumbwa na mizozo, majanga ya asili na uhamaji wa watu wengi, kwa haraka husaidia wale wanaohitaji katika sehemu nyingi za dunia, hasa katika nchi jirani kama vile Palestina na Syria, bila kujali lugha, dini, rangi au jinsia.
Uturuki imekuwa mojawapo ya nchi ambazo zimetoa misaada mingi zaidi ya kibinadamu kwa Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel. Katika muktadha huu, imewasilisha tani 102,000 za misaada ya kibinadamu kwa Gaza kwa njia ya bahari na anga tangu Oktoba 2023.
Usitishaji vita huko Gaza umetoa fursa ya kuwasilisha misaada endelevu na ya kutosha ya kibinadamu huko Gaza.
Kama muendelezo wa juhudi zake za usaidizi Gaza, Uturuki ilituma meli iliyobeba takriban tani 865 za misaada ya kibinadamu kutoka Bandari ya Mersin hadi Bandari ya El Arish nchini Misri mnamo Oktoba 14, 2025.
