UTURUKI
2 dk kusoma
Biashara kati ya Uturuki na Afrika yavuka dola bilioni 37, Ankara yalenga dola bilioni 40 mwaka 2026
Waziri wa Biashara wa Uturuki, Omer Bolat, amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Uturuki na Afrika kimevuka dola bilioni 37 mwaka 2024, huku Ankara ikilenga kufikia dola bilioni 40 ifikapo mwaka 2025.
Biashara kati ya Uturuki na Afrika yavuka dola bilioni 37, Ankara yalenga dola bilioni 40 mwaka 2026
Bolat alisema jumla ya biashara ya Türkiye na Afrika imeongezeka zaidi ya mara saba tangu 2003. / AA
16 Oktoba 2025

Akizungumza katika Mkutano wa 5 wa Biashara na Uchumi kati ya Uturuki na Afrika uliofanyika Alhamisi jijini Istanbul, Bolat alisema mkutano huo umefanyika wakati wa hali ya sintofahamu duniani, sera za kibiashara za kulinda masoko ya ndani, na changamoto kwa mfumo wa biashara wa kimataifa unaozingatia kanuni.

“Tunafurahi kuendeleza uhusiano wetu kwa kina na kimkakati katika nyanja za kiuchumi, biashara, utamaduni na kijamii kati ya Uturuki na nchi zote za bara la Afrika. Tunalenga kuendeleza uhusiano huo kwa misingi ya haki, usawa, utakaofaidisha pande zote, na tutaendelea kutekeleza sera hizi kwa imara zaidi,” alisema Bolat.

Alieleza kuwa jumla ya biashara ya Uturuki na Afrika imeongezeka kwa zaidi ya mara saba tangu mwaka 2003.

“Zaidi ya hayo, wakandarasi wa Kituruki pia wamechangia sana katika maendeleo ya Afrika kwa kushiriki katika miradi ya maendeleo 2,043 katika nchi mbalimbali za Afrika, na kukamilisha kazi za ujenzi zenye thamani ya karibu dola bilioni 100,” aliongeza.

Miradi mikuu

Bolat alisisitiza kuwa Shirika la Ndege la Uturuki, ambalo ndilo linalobeba bendera ya Uturuki, linaunganisha Afrika na dunia nzima kupitia Istanbul, kwa safari za ndege hadi vituo 62 katika zaidi ya nchi 40 za Afrika.

Aliongeza kuwa Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TIKA) na mashirika mengine ya misaada ya Uturuki yanaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kitamaduni, kijamii na kibinadamu katika bara zima.

"Takriban wafanyabiashara 3,000 kutoka nchi za Afrika wamejiandikisha na kuja hapa kuhudhuria mkutano huo. Maelfu ya wafanyabiashara wa Uturuki pia watakuwa hapa, kukutana na wenzao wa Afrika," Bolat alisema.

"Kutakuwa na vikao vya majadiliano kuhusu mada zaidi ya saba muhimu. Sita kati ya mawaziri wenzangu wa Uturuki watashiriki katika vikao hivo leo na kesho, na wako tayari kwa mikutano ya biashara baina ya nchi na nyinyi. Aidha, vikao vya biashara vitafanyika katika baadhi ya nchi," aliongeza.

Kongamano la 5 la Biashara na Kiuchumi la Uturuki-Afrika linafanyika katika Kituo cha Kongamano cha Istanbul mnamo Oktoba 16-17. Hafla hiyo imeandaliwa na Bodi ya Mahusiano ya Kiuchumi ya Kigeni (DEIK) kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika (AU) na kusimamiwa na Wizara ya Biashara ya Uturuki.

Katika kongamano hilo la siku mbili, vikao hivyo vitajadili kuhusu ushirikiano katika minyororo ya mauzo ya nguo, kufadhili mahitaji ya miundombinu ya Afrika, dawa na vifaa vya matibabu, kituo cha usafirishaji cha Uturuki-Afrika, uongozi wa wanawake na ujasiriamali, usalama wa chakula, nishati na madini, ushirikiano wa anga, na biashara ya kidijitali na tasnia.

CHANZO:TRT Afrika, TRT World