Waziri huyo amesema kuwa ushiriki wa Uturuki katika mipango ya ulinzi inayoongozwa na Ulaya, ikiwemo Mpango wa Usalama wa Ulaya (European Security Action Programme - SAFE), ni wa muhimu sana kwa usalama wa kikanda na wa kimataifa.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Guler alibainisha kuwa Uturuki ni miongoni mwa mataifa matano ya juu yanayochangia kwa idadi ya wanajeshi katika operesheni za NATO, na akaeleza msimamo wa Uturuki wa kuimarisha uwezo wake wa kijeshi kufuatia Mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa NATO na mkutano wa kilele wa Kikundi cha Mawasiliano cha Ulinzi cha Ukraine kilichofanyika Brussels.
Waziri huyo pia alisisitiza dhamira ya Ankara ya kuboresha jeshi lake kwa mifumo ya kisasa ya kijeshi, na kufikia lengo la uwekezaji wa ulinzi la asilimia 5 kama ilivyowekwa na NATO.
“Tulisisitiza mchango wetu kwa Ukraine katika ngazi ya pande mbili na ndani ya NATO, na msaada wetu kwa juhudi za kidiplomasia zinazolenga kusitisha mapigano na kuleta amani,” ilieleza taarifa hiyo.
Utayari wa kuchangia katika kikosi kazi cha Gaza
Waziri Guler pia alieleza kuridhishwa kwake na hali ya kusitishwa kwa mapigano Gaza, akisema kuwa hiyo ni fursa ya kufikia suluhisho la haki la mataifa mawili.
Alihimiza utekelezaji kamili wa makubaliano ya kusitisha mapigano na akasisitiza umuhimu wa misaada ya kibinadamu kuendelea bila kizuizi, huku akihaidi msaada zaidi kutoka Uturuki.
Guler pia alisema kuwa Jeshi la Uturuki liko tayari kushiriki katika kikosi kazi cha kimataifa Gaza, endapo misheni hiyo itaanzishwa.
Israel na Hamas walikubaliana kusitisha mapigano kwa makubaliano yaliyoongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump, yaliyolenga kumaliza zaidi ya miaka miwili ya vita vya kinyama vya Israel dhidi ya Gaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 60,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, waliuawa na Tel Aviv.
Uturuki ni mojawapo ya mataifa yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, pamoja na Marekani, Misri na Qatar.
Akiadhimisha zaidi ya miaka sabini ya uanachama wa NATO, Guler alisema kuwa Uturuki imeshirikisha misimamo yake ya kitaifa kuhusu masuala ya usalama wa kikanda na barani Ulaya na washirika wake.
Uturuki pia imesaini makubaliano ya mradi wa mafunzo ya kijeshi wa pamoja unaojulikana kama ‘Distributed Synthetic Training High-Visibility Project (HVP)’, unaolenga kujibu mahitaji yanayoongezeka ya mafunzo ya kijeshi ya kimataifa kwa njia ya gharama nafuu.