UTURUKI
1 dk kusoma
Viongozi wa Uturuki, Urusi wajadili kuhusu uhusiano wa mataifa mawili, kikanda, na masuala ya dunia
Recep Tayyip Erdogan amemwambia Vladimir Putin kwa njia ya simu kuwa juhudi za kidiplomasia ni muhimu kuimarishwa kuhakikisha vita vya Ukraine vinamalizika kwa "haki na amani ya kudumu."
Viongozi wa Uturuki, Urusi wajadili kuhusu uhusiano wa mataifa mawili, kikanda, na masuala ya dunia
Rais wa Uturuki pia alimtakia heri ya kuzaliwa Putin / AA
7 Oktoba 2025

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumanne walijadili kuhusu uhusiano wa mataifa mawili pamoja na masuala ya kikanda na dunia.

“Uturuki inafanya kazi kuhakikisha mapigano yanasitishwa Gaza, na kufikishwa kwa misaada katika kanda hiyo,” Erdogan alimwambia Putin kwa njia ya simu, kulingana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.

Erdogan anasema kuwa juhudi za kidiplomasia lazima ziimarishwe kuhakikisha kuwa vita vya Ukraine vinamalizika kwa “haki na amani ya kudumu,” akiongeza kuwa Uturuki pia itaendelea na juhudi zake za amani.

Rais wa Uturuki pia alimtakia Putin heri ya siku ya kuzaliwa.

Uturuki imewahi kuwa mwenyeji wa majadiliano ya ngazi za juu Machi 2022, wakati wajumbe wa Urusi na Ukraine walipokutana jijini Istanbul kwa mazungumzo ya moja kwa moja baada ya vita kuanza.

Huku mazungumzo hayo yakikwama, yalitoa njia ya makubaliano kama ya Nafaka za Bahari Nyeusi, ambayo Uturuki na Umoja wa Mataifa yalisaidia kuleta upatanishi.

Jiji la Istanbul pia limekuwa mwenyeji wa duru tatu za mazungumzo kufikia sasa — 16 Mei, 2 Juni na Julai 23 — yaliyolenga kufufua mazungumzo ya moja kwa moja ya kidiplomasia kati ya Urusi na Ukraine baada ya miezi kadhaa ya kukwama.

CHANZO:AA