Katika miaka ya sabini alifanya kazi na Shirika la Viwango Kenya na kuwa Naibu Mkurugenzi.
Mwaka 1982 alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini baada ya kuhusishwa na jaribio la mapinduzi lililoongozwa na wanajeshi ambao walinasibishwa naye.
Alifungwa jela na kuachiwa huru baada ya miaka sita lakini akakamatwa tena muda mfupi baadaye na kuachiwa miezi michache baadaye mwaka 1989.
Akakamatwa tena mwaka 1990 akiwa pamoja na wanaharakati wa wanasiasa waliokuwa wanapigania kuondolewa kwa mfumo wa utawala wa chama kimoja.
Aliachiliwa 1991 na akakikimbia nchi na kuelekea Norway akidai kuwa serikali ilikuwa inapanga njama ya kumuua.
Miaka kadhaa baadaye katika kitabu alichoandika kuhusu maisha yake ya siasa alikiri kuhusika katika jaribio hilo la mapinduzi kwa kiasi kikubwa.
Baadhi ya wanasiasa walitaka ashtakiwe tena kwa uhaini ila kisheria muda wa mashtaka kuanzishwa tena ulikuwa umepita.
Miongoni mwa waliofungwa pamoja naye wakati wa harakati zake za kutaka demokrasia ni wanasiasa Kenneth Matiba na aliyekuwa meya wa jiji la Nairobi Charles Rubia.
Raila Odinga alirejea nchini Kenya mwaka 1992 wakati huo akijiunga na chama alichokianzishwa baba yake Jaramogi Oginga Odinga, FORD na ndiyo mwaka ambapo uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ulifanyika nchini Kenya.
Raila alishinda ubunge wa jimbo la Langata, lakini baba yake hakufanikiwa kushinda urais dhidi ya Daniel arap Moi.