Umoja wa Afrika umekashifu jaribio lolote la mabadiliko ya serikali kinyume na katiba nchini Madagascar ambapo rais wa nchi hiyo Andry Rajoelina anaripotiwa kutimka kufuatia maandamano dhidi ya serikali yake.
Maandamano nchini humo yalianza Septemba 25 na yalichochewa kwa kukatika mara kwa mara kwa umeme na uhamba wa maji.
Baada ya muda, malalamiko yalibadilika na kujumuisha kupanda kwa gharama ya maisha, umaskini na madai ya ufisadi katika serikali, huku wengi wakimtaka Rajoelina ajiuzulu.
Kufuatia maandamano hayo, Rais Rajoelina alilazimika kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kumfuta kazi Waziri wa Nishati na kuvunja Baraza la Mawaziri mwishoni mwa mwezi Septemba, kwa matumaini ya kutuliza maandamano.
Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 22 wameuawa katika mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.
Nchi hiyo ina wakazi zaidi ya milioni 30, lakini takwimu zinaonyesha kuwa robo tatu ya raia wanaishi katika umaskini.
Madagascar imekumbwa na machafuko mengi tangu ilipopata uhuru mwaka 1960, yakiwemo maandamano makubwa mwaka 2009 ambayo yalimlazimu Rais wa wakati huo Marc Ravalomanana kuachia ngazi na Rajoelina kuingizwa madarakani.
Rajoelina mwenye umri wa miaka 51 alipoteza kuungwa mkono na CAPSAT, kikosi maalum cha jeshi ambacho kilimsaidia kuingia mamlakani katika mapinduzi ya 2009.
CAPSAT ilijiunga na waandamanaji mwishoni mwa juma, ikisema kuwa haiwezi kuwa sehemu ya mauaji ya raia.
Kikosi hicho baadaye kilisema kuwa kinasimamia jeshi na kumteua mkuu mpya wa majeshi.
Umoja wa Afrika umevitaka vitengo vyote vya Jeshi la Madagascar kuzingatia mamlaka yao ya kikatiba na kuacha kuingilia masuala ya kisiasa kwa mipango ya kuteua mjumbe atakaefuatilia kurudishwa kwa utulivu.
Baraza la Amani na Usalama la AU limetoa wito kwa waandamanaji kutumia njia zilizopo za kisheria kushughulikia malalamiko yoyote halali.
Rais wa bunge la seneti wakati wa maandamano aliondolewa na mwingine wa muda kuteuliwa.
Kulingana na katiba ya Madagascar, ikiwa ofisi ya rais itakuwa wazi, kiongozi wa Seneti anachukua wadhifa huo hadi uchaguzi ufanyike.
Kwa sasa haijulikani hatma ya Rais Rajoelina na ikiwa aterejea nyumbani na kwa upande mwingine hali ya kisiasa ya Madagascar itakuwaje na ni nani atachukua tena uongozi wa nchi hiyo?