Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema anajivunia kutekeleza dhamira ya mtangulizi wake, John Pombe Magufuli ya kuleta mabadiliko ndani ya nchi.
Akizungumza Oktoba 13, 2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika mkoani Geita, Samia amesema kuwa miradi mingi mikubwa ya maendeleo aliyoianzisha Magufuli ameikamilisha.
"Nyote mtakubaliana na mimi nimetekeleza dhamira yake na shauku yake ya kuleta mabadiliko ndani ya nchi yetu," alisema Samia.
Kulingana na Samia, mtangulizi wake alimuachia ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) ukiwa katika asilimia 37 na sasa amelikamilisha na kuzalisha umeme.
Alianisha mradi mwingine kuwa ni wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Dar es
Salaam hadi Morogoro ambao walianza pamoja, kabla ya kumuachia ukiwa asilimia 30, na sasa ameukamilisha na watu wanasafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na vipande kadhaa vinaendelea kujengwa hadi Kigoma.
Mgombea huyo wa CCM alisisitiza kuwa aliliacha daraja la Kigongo Busisi lilkiwa asilimia 21, lakini kwa sasa watu wanapita kwa saa chache kwenda upande mmoja kwa miguu na vyombo vya moto.
Samia amelitaja suala la Serikali kuhamia Dodoma kama mradi mwingine ambao ulianzishwa na Magufuli na sasa Serikali, Bunge na Mahakama vyote viko Dodoma, na Mji wa Serikali wa Mtumba unaendelea kukamilishwa.