Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga amefariki nchini India alipokuwa akipokea matibabu.
Raila anasifika kama mmoja wa viongozi wakongwe wa siasa nchini Kenya na anayefahamika kama mwanamageuzi.
Amekuwa nguzo muhimu katika siasa za nchi hiyo. Ana ushawishi mkubwa kwa wanaomuunga mkono na amekuwa na mchango mkubwa takriban katika kila serikali, licha ya yeye mara nyingi kuwa upande wa upinzani.
Wasifu wa Raila Odinga
Raila Amolo Odinga alizaliwa Januari 7 mwaka 1945. Amekulia katika mazingira ya siasa ambapo baba yake Mzee Jaramogi Oginga Odinga alikuwa mmoja wa wapigania uhuru wa Kenya na kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa taifa hilo.
Alikuwa kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha chini ya miaka miwili. Raila Odinga pamoja na baba yake walikuwa miongoni mwa wanasiasa waliopigania kuwepo kwa siasa za vyama vingi katika miaka ya themanini na tisini
Raila aliwahi kufungwa gerezani kwa kuhamasisha kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa. Amegombea urais mwaka 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022, kwa ujumla mara tano, ila hajapata fursa ya kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki, lakini amekuwa na mchango muhimu kwa kila serikali iliyokuwa madarakani.
Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2002, chama cha Raila kilijiunga na serikali ya rais wa awamu ya pili Daniel Arap Moi na akawa Waziri wa Nishati.
Mwaka 2002 akasaidia upinzani ulioongozwa na rais wa awamu ya tatu Mwai Kibaki kupata ushindi mkubwa dhidi ya Uhuru Kenyatta na chama cha KANU.
Licha ya kuwa nje ya serikali, mchango wake bado ulionekana baada ya maandamano ya vijana maarufu Gen Z, mwaka 2024, ambapo alionekana kufanya tena ‘’handshake’’ na serikali ya Ruto, hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa upinzani kujumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Raila Odinga alimuoa mke wake Ida Odinga, mwaka 1973 n apamoja walijaaliwa watoto wanne.