AFRIKA
2 dk kusoma
Takriban watu saba wauawa kwenye mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za RSF nchini Sudan
Angalau watu saba wmeuawa Jumanne kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyotekelezwa na Kikosi cha Wanamgambo wa RSF, nchini Sudan, kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo na wahudumu wa afya.
Takriban watu saba wauawa kwenye mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za RSF nchini Sudan
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, vilivyoanza Aprili 2023, vimeua maelfu ya watu hadi sasa. / / Reuters
tokea masaa 9

Utawala wa eneo la kaskazini wa mji wa Al-Dabbah ulisema kuwa watu watano waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya ndege isiyo ya rubani ya RSF kulenga majengo ya chuo katika mji huo.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama ya mji huo, Mohamed Saber Kashkash, aliishutumu RSF kwa kuendelea "kulenga maeneo ya raia."

Daktari mmoja na mwanawe pia waliuawa kwenye shambulio jingine la ndege isiyo na rubani katika Jimbo la East Nile, mashariki mwa Khartoum, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kikosi cha Sudan Shields, kundi linalounga mkono jeshi la serikali.

Vita vikali

Shambulio hilo lilitokea saa chache baada ya Mtandao wa Madaktari wa Sudan, kundi la madaktari wa ndani, kuishutumu RSF kwa kumuua daktari mwingine na kuwajeruhi wanawe wawili kupitia shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye nyumba yao katika eneo la Sharg En Nile, jijini Khartoum.

Vifo hivyo vipya vimefikisha jumla ya wahudumu wa afya waliouawa na kundi hilo la waasi tangu kuanza kwa vita nchini Sudan mwezi Aprili 2023 kuwa 233, kulingana na takwimu za mtandao huo.

Kundi hilo la madaktari limeitaka jumuiya ya kimataifa na mashirika ya haki za binadamu kuwawajibisha RSF kwa “uhalifu” wao wa mara kwa mara dhidi ya raia wa Sudan.

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF tangu Aprili 2023 yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kuwafanya takriban watu milioni 15 kuyakimbia makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za ndani.

Hata hivyo, utafiti kutoka vyuo vikuu vya Marekani unakadiria idadi ya vifo kufikia takriban 130,000.

CHANZO:AA