AFRIKA
2 dk kusoma
Rais wa Madagascar avunja bunge huku mzozo wa kisiasa ukitikisa nchi
Agizo lililowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook lilisema Rais Andry Rajoelina alishauriana na viongozi wa bunge na Seneti kuhusu uamuzi huo.
Rais wa Madagascar avunja bunge huku mzozo wa kisiasa ukitikisa nchi
Waandamanaji wakiandamana katika mji wa Antananarivo, Madagascar, Oktoba 13. / / Reuters
tokea masaa 11

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina siku ya Jumanne alivunja bunge, na hiyvo kupindua azma ya bunge kumuondoa madarakani, iliyoongozwa na upinzani, kutokana na mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Rajoelina amekabiliwa na zaidi ya wiki mbili za maandamano barabarani, yakiongozwa kwa kiasi kikubwa na waandamanaji vijana, na kumlazimisha kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 51 kujificha.

Agizo la kuvunja bunge "litaanza kutekelezwa mara moja baada ya kutangazwa kwenye redio na/au matangazo ya televisheni", ilisema taarifa ya rais katika ujumbe uliyowekwa kwenye Facebook.

Rajoelina, ambaye amekaidi wito unaoongezeka wa kumtaka ajiuzulu, alitetea hatua hiyo katika ujumbe tofauti kwenye mtandao wa kijamii kama muhimu "kurejesha utulivu ndani ya taifa letu na kuimarisha demokrasia."

"Lazima watu wasikike tena. Vijana wapewe nafasi," alisema kupitia mtandao wa kijamii.

Kumuondoa rais madarakani

Kiongozi wa upinzani Siteny Randrianasoloniaiko alisema Jumatatu watapiga kura kumshtaki Rajoelina kwa kukimbia kazini kufuatia ripoti kuwa aliikimbia nchi.

Rajoelina, meya wa zamani wa mji mkuu Antananarivo, alisema Jumatatu jioni alikuwa yuko "mahali salama" baada ya majaribio ya kumuua, bila kufichua eneo lake.

Maandamano hayo yalianza Septemba 25 na kufikia hatua muhimu mwishoni mwa juma wakati wanajeshi walioasi na vikosi vya usalama viliungana na waandamanaji hao na kumtaka rais na mawaziri wengine wa serikali kujiuzulu.

Miongoni mwao kulikuwa na kitengo cha CAPSAT, ambacho kilikuwa na jukumu kubwa katika mapinduzi ya 2009 ambayo kwanza yalimuweka Rajoelina madarakani.

Ili kujaribu kutuliza maandamano, rais mwezi uliopita alivunja serikali yake yote. Aliripotiwa kuhamishwa hadi Ufaransa kwa ndege ya kijeshi siku ya Jumapili baada ya makubaliano na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

CHANZO:AFP