Salamu za rambirambi zinatoka sehemu tofauti ya bara la Afrika baada ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga. Odinga ameaga dunia nchini India Jumatano, ambapo alikuwa anapata matibabu.
“Tumempoteza kiongozi mahiri, mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote.” ameandika Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika ukurasa wake wa X.
“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto, Mama Ida Odinga, watoto, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Kenya kwa msiba huu,” aliongeza kusema Rais Samia katika ujumbe wake mtandaoni.
Nae Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametoa ujumbe wake.
“Kwa niaba ya Serikali ya Ethiopia, natuma salamu zangu za rambirambi kwa kuondokewa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga. Apumzike Kwa amani,” Ahmed alisema katika akaunti ya X.
Nao uongozi wa Umoja wa Afrika pia umetoa salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho.
"Raila Odinga alikuwa mtu mashuhuri katika maisha ya kisiasa ya Kenya na mpiganaji thabiti wa demokrasia, utawala bora na maendeleo yanayozingatia watu. Ahadi yake ya miongo kadhaa ya haki, wingi wa watu na mageuzi ya kidemokrasia iliacha alama isiyofutika sio tu kwa Kenya bali katika bara zima la Afrika,” mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahamoud Ali Youssouf alisema.
“Alihamasisha vizazi vya viongozi, pamoja na imani yake, ujasiri na ustahimilivu wa raia. mazungumzo na taasisi za kidemokrasia,” alisema Mwenyekiti.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki naye ameandika rambirambi zake katika mtandawo wa kijamii.
“Ni kiongozi asiye na woga, Raila Odinga alitengeneza mkondo wa kisiasa wa nchi yake,” Faki alisema.
“Raila Odinga alitengeneza mkondo wa kisiasa wa nchi yake. Mtetezi mkubwa wa ushirikiano wa bara, pia aliitumikia kama Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu. Rambirambi zangu nyingi kwa familia yake,” aliongezea.