UTURUKI
3 dk kusoma
Wanaharakati wa Global Sumud wakosoa 'ugaidi wa Israeli', wapongeza uungwaji mkono wa Uturuki
Wanaharakati hao walipokelewa kwa furaha na serikali ya Uturuki wakati umati mkubwa wa watu ulipokusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul kuwakaribisha wanaharakati wa Global Sumud Flotilla.
Wanaharakati wa Global Sumud wakosoa 'ugaidi wa Israeli', wapongeza uungwaji mkono wa Uturuki
Wanaharakati wa Global Sumud Flotilla, wanaozuiliwa na Israel, wakikaribishwa mjini Istanbul. / AA
5 Oktoba 2025

Ndege iliyobeba wanaharakati wa Global Sumud Flotilla, ambao walishambuliwa na kukamatwa na Israel katika maji ya kimataifa, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul Jumamosi alasiri.

Wanaharakati hao walisema walikumbana na mateso yasiyo ya kibinadamu kutoka kwa mamlaka za Israel wakati wa kukamatwa, wakiongeza kuwa walinyimwa maji kwa siku tatu na hata hawakuruhusiwa kusali.

“Tangu meli zetu zilipoingia Gaza, tulikumbana na matusi kutoka kwa Israel; tulielewa vyema kile ambacho Wapalestina huko Gaza wanapitia, na hili linathibitisha kile ambacho Israel imekuwa ikifanya hadi sasa,” alisema mwanaharakati mmoja kwa TRT World.

Mwandishi wa habari wa Italia, Lorenzo Agostino, alisema kuwa alihisi yupo “mahali pa kinyama kabisa” wakati alipokamatwa kinyume cha sheria na Israel katika maji ya kimataifa baada ya shambulio la wiki hii dhidi ya meli za Global Sumud Flotilla zilizokuwa zikielekea Gaza.

Akizungumza na Anadolu baada ya kuwasili Istanbul kwa ndege maalum, Agostino alisema yeye na abiria wenzake walitekwa na kuwekwa katika hali za “fedheha.”

“Kisha walitupeleka nchi kavu, na mara tu tulipofika, walitenda kama kundi la kigaidi. Tulipigwa mateke, watu walinyimwa maji safi kwa zaidi ya siku mbili. Kwa ujumla, walitumia kila nafasi kutudhalilisha,” alisema.

Wanaharakati hao walipokelewa kwa shangwe na serikali ya Uturuki huku umati mkubwa ukikusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul kuwapokea wanaharakati wa Global Sumud Flotilla waliowasili kwa ndege maalum ya Shirika la Ndege la Uturuki.

Mwanaharakati wa Uturuki alisifu serikali ya Türkiye kwa msaada wake kwa Global Sumud Flotilla na kusema kwa TRT World, “Tulifanikiwa; tulivunja mzingiro wa kinyama wa Israel na kuonyesha jinsi Israel inavyokandamiza. Hili lilikuwa moja ya malengo yetu, na tumefanikiwa.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, aliwakaribisha wanaharakati hao, akiwapongeza kwa ujasiri na dhamira yao.

Alisisitiza juhudi zinazoendelea kuhakikisha kurejea haraka kwa raia wa Uturuki waliobaki.

Fidan alibainisha kuwa watu hawa wenye ujasiri wamechukua msimamo wa heshima dhidi ya ukandamizaji, wakawa sauti ya wanyonge kupitia mapambano yao ya haki na maadili ya kibinadamu.

Shukrani kwa Uturuki

Mwanaharakati wa Ufaransa, Yassine Benjelloun, ambaye alikuwa ndani ya Global Sumud Flotilla, alielezea jinsi walivyotendewa vibaya na kudhalilishwa na Israel wakati wa kukamatwa.

Alikuwa miongoni mwa wale waliolazimishwa kupelekwa Israel baada ya vikosi vya Israel kuwakamata katika maji ya kimataifa.

“Jinsi walivyotutendea (Israel) ni kwamba walituzuia kupata dawa kwa wale waliokuwa wakihitaji. Walitupa maji ya kunywa baada ya saa 32 tu,” Benjelloun alisema kwa Anadolu baada ya kuwasili Istanbul.

“Tulikuwa na chakula kidogo sana. Tuliamshwa saa 9 usiku na mbwa na wapiga risasi wakiingia vyumbani mwetu, wakituamsha kila baada ya saa mbili ili kutuzuia kulala,” alisema.

“Wanatutendea hivi, na inatufanya tuwaze tu kile wanachowafanyia Wapalestina.”

Benjelloun alitoa shukrani kwa Uturuki kwa kusaidia kurejea kwao salama.

“Tunapaswa kuishukuru Uturuki kwa kile walichofanya leo na kwa kuturudisha nyumbani salama.”

CHANZO:AA