Naibu Mwenyekiti na Msemaji wa Chama cha AK, Omer Celik, amelaani vikali matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, yaliyolenga kumshambulia Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, akisema kuwa matamshi hayo "hayana maana wala mashiko".
Kupitia ujumbe alioweka kwenye akaunti yake ya NSosyal siku ya Jumanne, Celik alimwelezea Netanyahu kama "kiongozi wa mtandao wa mauaji ya halaiki" na kumtuhumu kuwa na "ndoto ya mchana" kuhusu mji wa Jerusalem, ambao alisema ni thamani ya pamoja kwa wanadamu wote.
Celik aliongeza kuwa maneno ya Netanyahu ni ishara ya uadui dhidi ya maadili ya msingi wa kibinadamu na ni sawa na "jinai mpya ya mauaji ya halaiki dhidi ya watu na maadili yanayofanywa na misimamo mikali ya kupinga ubinadamu."
Akasema kuwa jibu la kweli linapaswa kutoka kwa "muungano wa kibinadamu" dhidi ya vitisho hivyo.
Awali, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alimshambulia vikali Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa shambulio la Israel dhidi ya kundi la wasuluhishi wa Hamas huko Qatar wiki iliyopita, akisema: "Kiitikadi, Netanyahu ni kama ndugu wa Hitler."
Erdogan aliongeza: "Kama ambavyo Hitler hakuweza kutambua kuwa kuna uwezekano wa kushindwa, Netanyahu atakumbana na hatima hiyo hiyo."
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akirejea kutoka Doha, ambako alihudhuria mkutano wa dharura wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kufuatia shambulio la anga la Israel katika nchi hiyo ya Ghuba.