UTURUKI
3 dk kusoma
‘Israel ni utawala unaofaidi kutokana na uharibifu na sio utulivu’ – Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki
Idara ya Mawasiliano ya Uturuki iliongoza mdahalo mjini Ankara katika jukwaa linaloitwa 'Gaza: The Litmus Test of Humanity.'
‘Israel ni utawala unaofaidi kutokana na uharibifu na sio utulivu’ – Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki
Duran alisema "jumuiya ya kimataifa haiwezi tena kupuuza ukweli wa uharibifu wa vitendo vya Israel." / / Wengine
17 Septemba 2025

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran, amesema kuwa “dunia inakumbwa na tatizo la Israel,” akielezea kuwa ni utawala wa uharibifu unaovunja sheria za kimataifa na “unaofaidi kutokana na uharibifu badala ya utulivu.

Duran amesema hayo siku ya Jumatano wakati wa mdahalo wa “'Gaza: The Litmus Test of Humanity.'” uliofanyika katika Idara ya Mawasiliano mjini Ankara na kuhudhuriwa na wanadiplomasia, wanaharakati wa elimu na wanahabari.

Katika hotuba yake, Duran alisisitiza msimamo thabiti wa Uturuki chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan: kutafuta usitishaji mapigano wa kudumu, kuhakikisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu, na kuanzisha taifa huru la Wapalestina na Yerusalemu Mashariki kama mji mkuu, ni mambo anayoyatilia umuhimu.

Alisisitiza kuwa “jamii ya kimataifa haiwezi tena kupuuza uhalisia wa uharibifu unaofanywa na Israel, ambao unatishia usalama wa kikanda na wa dunia nzima.”

Kuweka Gaza kwenye ajenda ya dunia

Duran alisisitiza jukumu kuu la Idara ya Mawasiliano ya Uturuki katika kuunga mkono Palestina kwenye “ngazi ya mawasiliano.”

Akielezea jinsi vyombo vyote vya kisasa vya habari na diplomasia vinavyotumika, alisema Idara hiyo inahakikisha “ukweli wa Gaza unabaki kwenye ajenda ya dunia.”

Alitaja juhudi mbalimbali kuanzia kufichua zaidi ya matukio 250 ya uongo unaosambazwa na Israel, kuchapisha majarida maalum, pamoja na kuandaa mikutano ya kimataifa, maonyesho na ziara za waandishi wa habari.

“Mawasiliano kwetu si zoezi la kiakili tu, bali ni suala la dhamiri,” alisema Duran.

“Tunajitahidi kuamsha dira ya maadili ya dunia na kuhakikisha kumbukumbu ya matendo ya Israel inahifadhiwa katika historia.”

Waandishi wa habari mstari wa mbele

Duran alitoa heshima maalum kwa vyombo vya habari vya Uturuki, akiwatambua TRT na Shirika la Habari la Anadolu kwa kazi zao kubwa za uandishi habari. Licha ya kukumbwa na vurugu na vizuizi, waandishi wa habari wa Uturuki “hawakuachana na jukumu lao kuwa sauti ya Gaza.”

TRT Haber ilitangaza zaidi ya ripoti 20,000 kutoka Gaza, na TRT World ilitenga nusu ya muda wake wa matangazo kwa Palestina na Gaza, alisisitiza.

Shirika la Habari la Anadolu lilitoa takriban habari 144,000 kwa lugha 13, pamoja na picha 200,000 na video 15,000, nyingi kati ya hizo sasa zinatumika kama ushahidi katika mchakato wa kisheria wa kimataifa.

Jukwaa la kidijitali la Uturuki, Tabii, lilianzisha sehemu iliyopewa jina “Simulizi za Wapalestina,” zinazopinga ukandamizaji katika huduma za kimtandao za kimataifa.

Idara ya Mawasiliano pia imemaliza kuchapisha kitabu kinachoandika habari za waandishi wa habari waliouawa Gaza, ikibainisha kuwa Israel iliwalenga kwa makusudi karibu waandishi wa habari 300 waliokuwa na jukumu la “kuripoti ukweli.”

“Harakati ya dhamiri”

Duran alikosoa ubaguzi wa nchi za Magharibi katika kuripoti habari, akiwahukumu vyombo vikubwa vya habari kwa upendeleo na kushiriki katika usambazaji wa habari potofu.

Akilinganisha, alielezea vyombo vya habari na taasisi za mawasiliano za Uturuki kuwa zinaongoza “harakati ya dhamiri” duniani.

“Vikosi vya Israel vinaweza kuvunja kamera za waandishi wetu,” Duran aligusia aliyoyasema Rais wa Uturuki, “lakini hawawezi kuzuia ukweli kufichuliwa.”

 

CHANZO:TRT World