UTURUKI
3 dk kusoma
Rais Erdogan wa Uturuki afanya vikao mbalimbali vya mataifa mawili jijini Doha
Rais wa Uturuki alikuwa na mazungumzo na viongozi wa Qatar, Saudi Arabia, Somalia, Syria na wa Iraq, pembezoni mwa mkutano wa ushirikiano wa nchi za Kiislamu na Kiarabu.
Rais Erdogan wa Uturuki afanya vikao mbalimbali vya mataifa mawili jijini Doha
Rais Erdogan wa Uturuki akiwa na viongozi mbalimbali jijini Doha, nchini Qatar./Picha: AA
15 Septemba 2025

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amefanya vikao na viongozi mbalimbali wakati wa mkutano wa ushirikiano wa nchi za Kiislamu na Kiarabu, jijini Doha nchini Qatar.

Mkutano huo, pia ulishuhudiwa kufikiwa kwa maamuzi kufuatia shambulizi la Septemba 9 lililofanywa na Israel jijini Doha na matendo mengine ya kidhalimu ya Israel yenye kuhatarisha umoja, huku Erdogan akionesha utayari wa Uturuki kuendelea kuisaidia Qatar na kulaani shambulio hilo dhidi ya timu ya usuluhishi la Hamas.

Qatar

Erdogan alimueleza kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, kuwa shambulizi la Israel dhidi ya Qatar halitokubalika na kusisitiza kuwa Uturuki itaendelea kusimama na Qatar.

Kulingana na Rais huyo, shambulio hilo limelenga kufifisha suluhu ya amani, akisisitiza haja ya kuendelea na mazungumzo katika hali yoyote ile, huku Uturuki ikiwa tayari kufanikisha mchakato wa maridhiano.

Aidha, aliongeza kuwa, uhusiano kati ya Uturuki na Qatar utaendelea kudumishwa katika nyanja tofauti, hususani sekta ya ulinzi na usalama.

Iraq

Wakati huo huo, Rais Erdogan wa Uturuki alimueleza Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al Sudani kuhusu kuendeleza uhusiano wa kupambana na ugaidi.

"Rais Erdogan aligusia haja ya kuendeleza uhusiano katika mapambano dhidi ya ugaidi na ushirikiano katika sekta za nishati na barabara kati ya Uturuki na Iraq," Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema.

Saudi Arabia

Wakati wa kikao chake na mwana wa mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, Erdogan alisema kuwa mashambulizi ya Israel “hayatokubalika”, na ni lazima Israel iwajibishwe kwa matendo yake, na kuwa Uturuki iko pamoja na nchi zinazolengwa na mashambulizi ya Israel, kulingana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.

Alibainisha kuwa Uturuki itaendelea na jiithada zake za kumaliza mgogoro wa Gaza na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

Somalia

Erdogan alimueleza kiongozi mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud umuhimu wa kuiwekea Israel vikwazo, kama hatua nzuri ya kuiwajibisha kiuchumi.

Kulingana na Erdogan, uhusiano kati ya Uturuki na Somalia, unakua siku kwa siku, akigusia utayari wa kuendelea kuisaidia Somalia.

Syria

Akiwa nchini Qatar, Erdogan alikutana na Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, na kuuita ushiriki wa Sharaa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuwa ni “jambo lenye umuhimu kihistoria”.

Kulingana na Rais wa Uturuki, nchi yake itaendelea kuisadia Syria na kuwa jitihada za kudumisha uhusiano wa nchi mbili, zilikuwa zikiendelea.

Aliongeza kuwa “Uturuki ilikuwa kwenye mchakato wa kuyaleta pamoja makundi mbalimbali nchini Syria, akisisitizia umuhimu wa kuenzi umoja wa Syria na mtangamano wake pamoja na SDF kuheshimu makubaliano ya Machi 10,” kulingana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.

 

 

CHANZO:TRTWorld