Uturuki itashiriki katika mchakato wa vikosi vya kimataifa ambavyo vitafuatilia utekelezaji wa kusitishwa mapigano Gaza, Rais Recep Tayyip Erdogan alitangaza siku ya Alhamisi.
Akisisitiza kuhusu jukumu la kidiplomasia la Uturuki katika kanda, Erdogan alisema Uturuki itafuatilia kwa karibu kutimizwa kwa makubaliano yote yaliyokubaliwa kuhusu kusitishwa mapigano na kuchangia kuhakikisha kuna usalama endelevu.
“Tutafanya kazi na jamii ya kimataifa kuunga mkono juhudi za ujenzi mpya na kusaidia kujenga tena Gaza,” Erdogan amesema, akisisitiza msaada wa Uturuki kwa watu na kujihusisha kisiasa katika mchakato wa baada ya kusitishwa mapigano.
Rais wa Uturuki ameeleza hali ilivyo Gaza kuwa “mauaji ya halaiki,” akiongeza kuwa lengo la Uturuki ni kusitisha umwagikaji damu na kurejesha amani katika kanda haraka iwezekanavyo.
“Lengo letu ni kusitisha mauaji ya halaiki Gaza na kuleta amani katika kanda haraka iwezekanavyo,” Erdogan amesema. Pia alisisitiza kuwa watu wa Palestina wamepitia madhila na mateso ya muda mrefu na kwamba dunia isisahahu kuhusu madhila yao.
“Hakuna mtu yoyote duniani ambaye anahitaji amani, usalama, na uthabiti zaidi ya watu wa Gaza,” aliongeza.