AFRIKA
3 DK KUSOMA
Kenya kuondoa paa za asbesto ndani ya miezi mitatu
Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, NEMA, ilitengeneza miongozo ya kitaifa kuhusu usimamizi salama na utupaji wa asbestosi mnamo 2011 kabla ya kufanyiwa marekebisho mwaka wa 2013.
Kenya kuondoa paa za asbesto ndani ya miezi mitatu
Rwanda ni kati ya nchi ambazo imeondoa asbesto / Picha kutoka Mamlaka ya Nyumba ya Rwanda   / Others
29 Agosti 2024

Serikali ya Kenya imeamuru paa za asbesto kuondolewa katika nyumba nchini humo.

Asbesto ni madini ya kiasili yanayoundwa na nyuzi ndogo ndogo na kutumika kutengezea paa za nyumba.

Waziri wa Mazingira Aden Duale aliamuru kuondolewa kwa paa hizo kutoka katika majengo yote nchini ndani ya miezi mitatu.

Waziri huyo alitaja hatari za kiafya na kuonya kuhusu uwezekano wa kufunguliwa mashtaka kwa wale watakaokaidi amri hiyo.

Duale aliiagiza Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira kuziandikia taasisi hizo ili kuondoa madini hayo hatari.

Katika miaka ya 1960 na 1970, asbesto ilikuwa nyenzo maalumu katika sekta ya ujenzi.

"Tumeiandikia Wizara za Ulinzi, Usalama wa Ndani, Elimu na Afya kufanya ukaguzi wa vituo vyote vinavyoezekwa kwa asbesto," Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, NEMA Mamo Mamo alisema.

Vifaa kadhaa ikiwemo viwanda vya kutengeneza chakula na nyumba za makazi zilitumia asbesto kuezeka kutokana na uimara wake na sifa za kustahimili moto.

Nyuzi za asbesto zina nguvu na sifa ya kustahimili joto. Bidhaa nyengine nyingi zina asbesto.

Kwa nini Asbesto ni hatari?

Wakati asbesto inaposumbuliwa, ama katika hali yake ya asili au katika bidhaa iliyo na asbesto, nyuzi hizi zinaweza kuingia hewani na kuvutwa kwa urahisi mtu anapopumua.

Nyuzi za asbesto zinaweza kunaswa kwenye mapafu, na hivyo kusababisha magonjwa kadhaa ya kutishia maisha kama saratani.

Nyuzi za asbesto mwilini huongeza hatari ya kupata saratani ya mapafu, uzazi na maeneo ya kuvutia hewa kwenye shingo na mapafu.

Saratani hizi mara nyingi hukua miongo kadhaa baada ya mtu kupumua asbesto kwa muda.

Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, NEMA, ilitengeneza miongozo ya kitaifa kuhusu usimamizi salama na utupaji wa asbestosi mnamo 2011 kabla ya kufanyiwa marekebisho mwaka wa 2013.

Miongozo hiyo ilitolewa kupitia juhudi za mashauriano na za pamoja za NEMA na mashirika yanayoongoza kama vile Wizara ya Afya, Kurugenzi ya Usalama na Huduma za Afya Mahali pa Kazi na iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Nairobi.

Katika nchi jirani ya Rwanda, juhudi za kuondoa asbesto yote nchini zinaendelea. Kufikia Februari 2024, Mamlaka ya Nyumba ya Rwanda ilitangaza kuwa zaidi ya asilimia 84 ya paa zilizo na asbesto zimeondolewa.

Mpango huo ulianza mwaka wa 2011.

CHANZO:TRT Afrika