Bunge la Afrika Mashariki (EALA) limechagua wajumbe maalumu ndani ya Jumuiya hiyo watakaoshughulikia uwazi na uwajibikaji.
Uchaguzi huo umefanyika katika kikao cha bunge hilo kilichofanyika katikati ya wiki jijini Arusha, Tanzania.
Wajumbe hao maalumu walioteuliwa ni mbunge kutoka Rwanda, Clement Musangabatware ambaye atakuwa ni rais wa mtandao huo unaofahamika kama EAPNAC, huku makamu wake akiwa Jesang Kering kutoka Kenya.
Uganda itawakilishwa na Babirye Veronica ambaye pia ni mweka hazina wa mtandao huo, wakati Jeremiah Odok kutoka Sudan Kusini atakuwa Katibu Mkuu wa mtandao huo.
Kwa upande mwingine, mtandao huo utahusisha viongozi wa matawi katika nchi wanachama wa EAC, ambao ni Dkt.Gladness Salema (Tanzania), Mugyenyi Mary Rutamwebwa (Uganda), Kalonzo Kennedy Musyoka (Kenya), Matthias Harebamungu (Rwanda), Nkurunziza Olivier (Burundi), Ngate Mangu Francois (DRC) na Ayason Mukulia Kennedy (Sudan Kusini).
“EAPNAC itaendelea kuwa sauti ya kuhakikisha kuwa mali za umma zinasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji ndani ya jumuiya yetu,” alisema Musangabatware.
Rais huyo wa EAPNAC alisisitiza haja ya kufanya kazi kwa pamoja kujenga mifumo ya kuzuia mianya ya rushwa na kukuza uwajibikaji ndani ya jumuiya ya EAC.