Rais wa Kenya, William Ruto, ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha kiongozi wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, na kusema kwamba Odinga atapewa mazishi ya heshima za kitaifa.
Odinga, mwenye umri wa miaka 80, aliripotiwa kuanguka ghafla wakati wa matembezi ya asubuhi ndani ya eneo la kituo cha tiba cha Ayurvedic kilichoko Koothattukulam, India, na baadaye alipelekwa hospitalini ambapo alitangazwa kufariki dunia saa 3:52 asubuhi kwa saa za Kenya.
Katika hotuba yake ya kitaifa Jumatano, Rais Ruto alimpongeza Odinga kwa kusema alikuwa "kiongozi jasiri" na mwanafalsafa wa siasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya kwa miongo kadhaa.
“Kuheshimu mchango wa kipekee wa mheshimiwa Raila Odinga kwa taifa letu, nimetangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa cha siku saba ambacho bendera ya kitaifa itashushwa nusu mlingoti kote nchini Kenya na katika ofisi zetu zote za nje ya nchi,” alisema Ruto.