AFRIKA
2 dk kusoma
Watu wanne wafariki dunia kufuatia majaribio ya vikosi vya usalama kuwatawanya waombolezaji wa Raila
Watu wanne wamefariki dunia jijini Nairobi, Kenya, siku ya Alhamisi baada ya vikosi vya usalama kufyatua risasi na kurusha mabomu ya gesi kuwatawanya maelfu ya watu waliokusanyika kwenye uwanja wa Kasarani kuuaga mwili wa Raila Odinga.
Watu wanne wafariki dunia kufuatia majaribio ya vikosi vya usalama kuwatawanya waombolezaji wa Raila
Umati mkubwa ulifurika barabarani na kujaribu kuingia bungeni, ambako awali serikali ilikuwa imepanga kuweka mwili wa Odinga. / / Reuters
tokea masaa 4

Odinga, ambaye alikuwa ni sura maarufu katika siasa za Kenya kwa miongo kadhaa — aliwahi kuwa mfungwa wa kisiasa na kugombea urais mara tano bila mafanikio — alifariki dunia siku ya Jumatano akiwa na umri wa miaka 80 nchini India, ambako alikuwa akipokea matibabu.

Maelfu ya wafuasi wake walijitokeza barabarani tangu asubuhi, lakini hali ya taharuki ilitokea baada ya umati mkubwa kuvunja lango la kuingia uwanja mkuu wa michezo wa Nairobi. Kulingana na ripoti kadhaa wanajeshi walifyatua risasi hewani kujaribu kutuliza hali hiyo.

Chanzo kutoka polisi kiliiambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wawili walipigwa risasi na kufariki dunia. Hata hivyo, vituo vya habari vya KTN News na Citizen TV nchini Kenya viliripoti kuwa idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watu wanne, huku wengi wakijeruhiwa.

Baada ya kufyatuliwa kwa risasi, polisi walirusha mabomu ya gesi na kuwatawanya maelfu ya waombolezaji.

Umati mkubwa pia ulifurika barabarani na kujaribu kuingia bungeni, ambako awali serikali ilikuwa imepanga kuweka mwili wa Odinga kwa ajili ya kuagwa na umma.

Ingawa anafahamika zaidi kama kiongozi wa upinzani, Odinga aliwahi kuwa Waziri Mkuu mwaka 2008, na mwaka jana alifanya makubaliano ya kisiasa na Rais Ruto — katika maisha ya kisiasa yaliyojaa miungano ya kila aina.

Alikuwa na wafuasi waaminifu mno, hasa kutoka jamii ya Waluo ya magharibi mwa Kenya, ambao wengi wao wanaamini aliibiwa ushindi wa urais kutokana na wizi wa kura.

Waombolezaji wa Odinga, wengi wao wakiwa vijana ambao hawakuwa hata wamezaliwa mwaka 1991 wakati Kenya ilipoanzisha mfumo wa vyama vingi, walimuenzi kama shujaa wa mageuzi ya kidemokrasia.

InayohusianaTRT Afrika - Mwili wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, umewasili Nairobi kutoka India

CHANZO:Reuters