Simanzi imetawala nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla, kufuatoa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Amolo Odinga.
Odinga, mwenye umri wa miaka 80, amefariki dunia nchini India, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Raila, maarufu kama ‘RAO’, atakumbukwa kwa ushawishi wake aliokuwa nao kwenye ulingo wa siasa ndani na nje ya Kenya.
Mwanasiasa huyo, aliyezaliwa Januari 7, 1945, amekuwa nguzo muhimu katika historia ya siasa ya nchi hiyo.
Raila, ambaye pia alifahamika kwa jina la ‘Tinga’, amekuwa nguzo muhimu katika siasa za nchini Kenya kutokana na harakati zake za siasa ambazo zimedumu kwa zaidi ya miaka 40.
Kwa kiasi fulani, unaweza kusema kuwa amerithi harakati hizo kutoka kwa baba yake mzazi, Hayati Jaramogi Oginga Odinga, ambaye alikuwa mmoja wa wapigania uhuru wa Kenya na baadaye kuja kuwa Makamu wa Kwanza wa taifa hilo.
Ni harakati hizo hizo, ambazo zilimfanya afungwe jela kwa nyakati tofauti.
Raila, ambaye alipenda kujifananisha na Cesc Fabreags, kiungo mchezeshaji wa zamani wa klabu ya Arsenal, akisisitiza kuwa yeye ni kiungo muhimu katika kutengeneza safu ya uongozi mahiri nchini Kenya.
Mwanasiasa huyo aliwahi kugombea nafasi ya Urais vipindi vitano tofauti, bila mafanikio yoyote.
Licha ya hali hiyo, RAO amekuwa na nafasi na mchango wa pekee kwenye siasa za Kenya.
Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2002, chama cha Raila kilijiunga na serikali ya rais wa awamu ya pili Daniel Arap Moi, huku yeye akipewa nafasi ya Uwaziri wa Nishati.
Mwaka 2002 akasaidia upinzani ulioongozwa na rais wa awamu ya tatu Mwai Kibaki kupata ushindi mkubwa dhidi ya Uhuru Kenyatta na chama cha KANU.
Kugombea Urais
Mwaka 2007 aligombea nafasi ya Urais dhidi ya Mwai Kibaki, ambapo alishindwa na Kibaki, katika matokeo yaliyozua vurugu kubwa baada ya uchaguzi.
Ili kuleta mapatano ndani ya nchi hiyo, Raila ‘akatengenezewa’ nafasi ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Raila aligombea nafasi ya Urais mara mbili; mwaka 2013 na 2017, dhidi ya Uhuru Kenyatta, bila mafanikio yoyote.
Mwaka mmoja baadaye, RAO na Uhuru Kenyatta wakaingia kwenye makubaliano maarufu kama “handshake”, kwa ahadi ya kufanya kazi pamoja na baada ya hapo, Uhuru kumuunga mkono ‘Baba’ katika harakati zake wa kuwania Urais.
Hata hivyo, Raila alipoteza nafasi ya Urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2022, aliposimama dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Uhuru Kenyatta, William Ruto.
Licha ya kuwa nje ya serikali, mchango wake bado ulionekana baada ya maandamano ya vijana maarufu Gen Z, mwaka 2024, ambapo alionekana kufanya tena “handshake” na serikali ya Ruto, hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa upinzani kujumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Nje ya Siasa
Mbali na siasa, Raila alipenda kusikiliza muziki aina ya Reggae na alikuwa shabiki wa timu ya Arsenal ya nchini Uingereza.
Ameacha mjane, Ida Odinga na watoto watatu Rosemary Odinga, Winnie Odinga na Raila Odinga Jr.