Umoja wa Afrika (AU) umesimamisha kwa muda uanachama wa Madagascar saa chache baada ya kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi kutangaza kuwa ataapishwa kama sais wa nchi hiyo.
"Utawala wa sheria lazima ushinde dhidi ya utawala wa nguvu," alisema Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahamoud Ali Youssouf, katika taarifa yake Jumatano, akibainisha kuwa utekelezaji wa hatua hiyo unaanza mara moja.
Rais Andry Rajoelina alikimbia nchi kwa kuhofia usalama wake baada ya wiki kadhaa za maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na kizazi cha "Gen-Z," ambayo yaliungwa mkono na vikundi vya kijeshi kutokana na uhaba wa maji na umeme. Hatua yake ya kuvunja serikali nzima iliongeza shinikizo la kumtaka ajiuzulu.
Kutoka eneo lisilojulikana, alijaribu kuvunja Bunge la Kitaifa kwa amri ya rais.
Hata hivyo, Bunge la Kitaifa lilikataa amri hiyo na kupiga kura ya kumuondoa madarakani Jumanne.
Muda mfupi baadaye, Kanali Michael Randrianirina na kikosi chake maalum cha kijeshi cha CAPSAT walitangaza kuwa jeshi limechukua mamlaka, kuvunja taasisi nyingi za serikali, na kuanzisha serikali ya mpito.
Randrianirina aliwaambia waandishi wa habari mapema Jumatano kuwa atakula kiapo hivi karibuni kama rais baada ya Mahakama Kuu ya Katiba kumwalika kushika nafasi hiyo.
Pia Jumatano, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ilichagua jopo la wazee kwa lengo la kupunguza mvutano katika koloni la zamani la Ufaransa.
Rais wa Malawi, Peter Mutharika, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama, alisema katika taarifa kuwa Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda, ataongoza jopo hilo katika juhudi za kuleta utulivu, amani, na mazungumzo katika taifa hilo la kisiwa.
"Hakuna maisha zaidi ya Wamalagasy yanayopaswa kupotea kutokana na machafuko haya," alisema Mutharika.