Unajua kuwa hati ya kwanza ya kusafiria ya Raila Odinga ilitolewa jijini Dar es Salaam mwaka 1962 katika nchi iliyofahamika kama Tanganyika?
Ni hati hiyo hiyo, iliyotumiwa na Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya kuingia Ujerumani Mashariki kwa ajili ya masomo yake ya elimu ya juu.
Pasipoti hiyo ya muda ilitolewa kwa Raila na vijana wengine wawili, kabla ya Tanganyika kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuzaliwa Tanzania.
Kulingana na Raila mwenyewe, hii ilitokana na kwamba idara ya uhamiaji ya Kenya ambayo ilikuwa chini ya Uingereza kwa wakati huo, kumnyima hati ya muhimu, na badala yake, Waziri Mkuu wa Tanganyika kwa wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alikuwa swahiba wa baba mzazi wa Raila, Jaramogi Oginga Odinga, kumpatia pasipoti hiyo kutoka Tanganyika.
Hii ni kwa mujibu wa simulizi inayopatikana katika kitabu chake cha ‘The Flame of Freedom’ kilichozinduliwa mwaka 2013.
Raila, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17, wakati huo akiwa kidato cha pili, alitakiwa aende kusoma nje ya nchi, kutokana na mahusiano mazuri kati ya Jaramogi Odinga na nchi za Umoja wa Kisoveti, tofauti na ilivyokuwa kwa serikali ya Uingereza.
Kwa upande wake, kaka yake mkubwa, Oburu Odinga ambaye alikuwa ameshatangulia kuelekea kwenye umoja wa nchi za Kisovieti, hakunyimwa tu fursa ya kujiunga na shule nzuri za Kenya, bali pia alinyimwa pasipoti ya kumwezesha kwenda nje ya nchi.
“Ombi la Oburu lilikataliwa mapema kabisa, kwa kisingizio kwamba pasipoti ya Jaramogi ilikuwa ikishikiliwa na serikali kwa sababu alikuwa ametembelea nchi za Kisoveiti na China. Kwa wakati huo, Jaramogi alikuwa akitumia pasipoti za kimataifa alizopewa na Kwame Nkrumah na Gamal Abdiel Nasser,” anasema Raila katika kitabu hicho.
Anaongeza: Katika kipindi hicho, Jaramogi alijua kwamba ili tupate elimu nzuri, basi ilitupasa tukasome nje ya nchi.
Kulingana na Raila, mmoja wa wasaidizi wa baba yake aitwaye Okuto Bala, alimchukua kutoka shule ya sekondari Maranda iliyopo Nyanza na kupelekwa Nairobi, kisha Dar es Salaam.
“Kipindi hicho barabara ya lami kutoka jiji la Nairobi iliishia njia panda ya uwanja wa ndege…kutoka hapo mpaka Namanga ilikuwa ni vumbi. “Tulipitia Korogwe, Handeni na kisha Morogoro ambapo lami ilianza tena.”
Kwa mujibu wa Raila, walifika Dar es Salaam saa moja na nusu asubuhi, na saa 24 baadaye, walipokelewa na Dola Osman, aliyekuwa msaidizi binafsi wa Katibu Mkuu wa chama cha TANU, Oscar Kambona.
“Tulikaribishwa vizuri, tukawekwa hotelini na baada ya kuoga na kubadilisha mavazi yetu, Osman alikuja kutupokea na kuchukua picha zetu tatu za pasipoti,” anaeleza Raila.
Baada ya hatua kadhaa za kushughulikia pasipoti zao, Raila na kaka yake walipata fursa ya kutembelea jiji la Dar es Salaam kabla ya kukutana na Mwalimu Nyerere.
“Mwalimu alifurahi sana kutuona, alituambia kuwa alikuwa rafiki mzuri wa Jaramogi…tulipata mlo pamoja na Mwalimu Nyerere, kabla hajatutakia safari njema na masomo mema,” anasema Raila katika kitabu hicho.