Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Jumatatu ilimtia hatiani kiongozi wa kwanza wa wapiganaji kuwahi kufikishwa mahakamani kwa ukatili alioufanya katika jimbo la Darfur nchini Sudan zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Mahakama imempata Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman na hatia ya makosa 27 ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji na mateso.
Hukumu yake itatolewa baadaye baada ya hatua nyingine kusikilizwa.
Hukumu katika kesi ya kwanza na ya pekee inayohusu uhalifu nchini Sudan tangu kesi hiyo kupelekwa mahakamani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2005 ni ishara ya kihistoria kwa ICC.
Bado kuna hati za kukamatwa kwa maafisa wa Sudan, ikiwa ni pamoja na mmoja anayemtuhumu Rais wa zamani Omar al-Bashir kwa mashtaka ya mauaji ya halaiki.
Kukamatwa kwake
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, ambaye pia anajulikana na nom de guerre Ali Kushayb, anakabiliwa na makosa 31 ya uhalifu ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji na mateso yanayodaiwa kutekelezwa huko Darfur kati ya Agosti 2003 na angalau Aprili 2004.
Waendesha mashtaka wanasema alikuwa kiongozi wa wapiganaji maarufu wa Sudan wa Janjaweed, ambao walishiriki "kwa nguvu" katika uhalifu wa kivita.
Lakini Abd-Al-Rahman, ambaye alizaliwa mwaka 1949 amekana mashtaka yote akiiambia mahakama kwamba wamepata mtu ambaye siye wanaemtafuta.
"Mimi sio Ali Kushayb. Simjui mtu huyo... sina uhusiano wowote na mashtaka dhidi yangu," aliiambia mahakama katika kikao cha Disemba 2024.
Abd-Al-Rahman alikimbilia Jamhuri ya Afrika ya Kati Februari 2020 wakati serikali mpya ya Sudan ilipotangaza nia yake ya kushirikiana na uchunguzi wa ICC.
Alisema baada ya hapo alijisalimisha kwa sababu alikuwa "amekata tamaa" na alihofia viongozi wangemuua.
"Nilikuwa nikisubiri kwa muda wa miezi miwili nikiwa mafichoni, nikizunguka kila sehemu, na nilionywa kuwa serikali inataka kunikamata, na niliogopa kukamatwa," alisema.
Mapigano yalizuka katika jimbo la Darfur nchini Sudan wakati makabila yasiyo ya Kiarabu, yakilalamikia ubaguzi wa kimfumo, yalichukua silaha dhidi ya serikali inayotawaliwa na Waarabu.
Khartoum ilijibu kwa kuwaachilia Janjaweed, kikosi kilichotolewa kutoka miongoni mwa makabila ya kuhamahama ya eneo hilo.
Umoja wa Mataifa unasema watu 300,000 waliuawa na milioni 2.5 walikimbia makazi yao katika mzozo wa Darfur kwenye miaka ya 2000.