AFRIKA
2 dk kusoma
Tembo 500 wahamishwa nchini Tanzania
Zoezi hilo, linakuja baada ya wataalamu wa Ikolojia kutoka shirika hilo kuyafuatilia makundi hayo kwa ukaribu zaidi.
Tembo 500 wahamishwa nchini Tanzania
Makundi ya tembo yakihamishwa kutoka Kyerwa na Karagwe kuelekea Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato nchini Tanzania./Picha:TANAPA
tokea masaa 16

Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikisha uhamishaji wa tembo takribani 500 kutoka katika maeneo ya wananchi na mwekezaji wilayani Kyerwa na Karagwe kuelekea Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato.

Zoezi hilo endelevu, ambalo linatekelezwa kitaalamu kwa ushirikiano kati ya TANAPA na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lilihusisha uhamishwaji wa makundi makubwa mawili yenye tembo zaidi ya mia 100, waliotembea umbali wa zaidi ya kilometa 150 kutoka Kyerwa kuelekea ndani ya Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato.

Zoezi hilo, linakuja baada ya wataalamu wa Ikolojia kutoka shirika hilo kuyafuatilia makundi hayo kwa ukaribu zaidi.

“Zoezi linaendelea vizuri licha ya changamoto kadhaa zinazojitokeza kwa tembo wakorofi ambao hujitenga na wenzao, pia endeleeni kuyafuatilia yale makundi ambayo mmeshayafikisha hifadhini ili yasirudi tena na kwenda kusababisha karaha kwa wananchi na mali zao japo kwa umbali waliotembea na misukosuko waliyoipata ni vigumu kurudi, ila tuendelee kuwachunguza kwa ukaribu,” alisema Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Massana Mwishawa.

Mchakato huo wa kuwaswaga tembo, ulihusisha helikopta mbili za JWTZ na magari kadhaa, ambapo hadi kufikia Oktoba 3, 2025 zaidi ya tembo 105 waliokuwa katika makundi mawili, waliswagwa kutoka Kyerwa yalipo mashamba ya mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari (Kagera Sugar) hadi eneo liitwalo Golini ulipo mpaka wa wilaya ya Kyerwa na Karagwe kuelekea Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato.

Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa Fredrick Mofulu alisema kuwa watahakikisha tembo wote waliosalia wanahamishwa ili kumaliza kabisa adha waliyokuwa wakiipata wananchi ya kuharibiwa mazao yao na kuhatarishiwa maisha yao na wanyamapori hao.

Zoezi hili pia limeshirikisha taasisi nyingine za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zikiwemo taasisi za Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mkoani Kagera.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili